Rais Paul Kagame wa Rwanda |
Chama tawala nchini Rwanda kimempitisha Rais Paul Kagame
kuwa mgombea wake katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 4.
Mapema Jumamosi Juni 17, wajumbe 1929 kati ya 1930 wa
mkutano mkuu wa chama chake cha RPF-Inkotanyi waliamua kumchagua tena kuwania
kiti cha urais wa nchi hiyo.
Kagame amelitawala taifa hilo tangu mwaka 2000. Katika mkutano
huo wa Jumamosi Kagame alikuwa mgombea pekee.
Anatarajiwa kupata upinzani kidogo kutoka kwa wagombea
wanaowakilisha vyama vidogo au wagombea huru.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 59 alikubali uteuzi huo
na kuahidi kuendelea kuiongoza nchi hiyo kuelekea kwenye ustawi, amani na
uthabiti zaidi.
“Sasa kwa kuwa mmenileta hapa kukubali, nimelipokea. Nitatumia
uwezo wangu wote” rais huyo aliwaambia wajumbe wa RPF na wawakilisha kutoka
vyama tisa vingine vilivyoalikwa kwenye mkutano huo.
“Kuna jambo muhimu hapa. Sio tu kuwa rais. Sio tu kuwa
na haki ya kuwa rais. Rwanda inataka na inahitaji rais sahihi,” aliongeza.
Kati ya vyama 11 vya kisiasa vilivyosajiliwa nchini
humo, vyama 9 vimesema kuwa vitamuunga mkono Kagame badala ya kuweka wagombea.
Uamuzi wa Kagame kugombea awamu ya tatu unakuja baada ya
nchi hiyo kufanya mabadiliko ya katiba katika kura ya maoni ya mwaka 2015,
ambayo yalimruhusu kugombea muhula mwingine wa miaka saba na kisha mihula
miwili ya miaka mitano mitano.
Hiyo ina maana kuwa Kagame anaweza kubaki madarakani
mpaka mwaka 2034.
Wapinzani nchini humo waliita kura hiyo ya maoni kuwa
isiyokuwa ya kidemokrasia, huku Marekani ambayo ni mshirika muhimu wa Rwanda,
ikipinga uamuzi wa Kagame kubaki madarakani.
0 comments:
Post a Comment