Rais wa Rwanda, Paul Kagame amechaguliwa kuwa mwenyekiti
wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele cha umoja huo unaofanyika katika
mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Bwana Kagame anapokea kijiti hicho cha uongozi kutoka
kwa Rais wa Guinea, Alpha Conde. Ataongoza umoja huo kwa muhula wa mwaka mmoja.
Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi huo, Kagame alizitaka
nchi za Afrika kuungana, kuunda soko la pamoja la Afrika, kuunganisha
miundombinu na kushirikisha uchumi na teknolojia.
Ili kufanikisha malengo yake, Kagame aliwataka viongozi
wa Afrika kumuunga mkono.
“Ahsanteni kwa imani yenu kubwa. Kwanza kama kiongozi wa
mchakati wa mabadiliko na sasa kama mwenyekiti wa umoja wetu.” Kagame alisema.
“Ninaahidi kufanya kazi bora. Lakini ninahitaji mniunge mkono kikamilifu.”
Kagame anatumai kuona umoja huo ukijitegemea na kuacha
kuwa tegemezi baada ya uamuzi uliofanywa kwamba nchi zote wanachana zitenge
asilimia 0.2 ya kodi ya bidhaa kutoka nje kufadhili shughuli za umoja huo.
Afrika “inakaribia” kuwa na eneo huru la biashara”,
alisema mwenyekiti huyo mpya. “Ukweli hilo linatakiwa kufanyika mwaka huu.”
0 comments:
Post a Comment