Kiongozi wa Kuwait Sheikh Sabah al-Ahmad Al-Sabah (mbele) akihudhuria ufunguzi wa mkutano wa 38 wa viongozi wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) kwenye kasri la Bayan mjini Kuwait, mnamo Desemba 5, 2017. |
DOHA, Qatar
Mlolongo wa ziara
zinazotarajiwa kufanywa na viongozi wa mataifa ya Ghuba nchini Marekani
unaonekana kuwa unalenga kutengeneza mazingira mazuri ya mkutano mkubwa kati ya
Marekani na Ghuba unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei.
Kwa mujibu wa
maafisa wa ngazi za juu wa Kiarabu, mkutano huo unalenga kutanzua mgogoro wa
kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa kati ya Qatar na na mataifa manne ya Kiarabu
yakiongozwa na Saudi Arabia.
Mrithi wa kiti cha
Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman, anatarajiwa kufanya ziara mjini
Washington mnamo Machi 19. Mwezi mmoja baadaye kiongozi wa Qatar, Tamim bin
Hamad Al Thani naye anatarajia kufanya ziara kwenye mji mkuu huo wa Marekani.
Akizungumza kwenye
televisheni ya taifa mapema Jumatano, Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Kuwait Khaled
al-Jarallah alisema kuwa ziara hizo zinalenga kuandaa mazingira kwa ajili ya
mkutano huo.
"Kuna matumaini
ya kufanyika mkutano wa kilele nchini Marekani kwa lengo la kutanzua mgogoro wa
uhusiano kati ya mataifa ya Kiarabu," alisema bwana al-Jarallah. "Lakini
mialiko bado haijatumwa."
"Mgogoro huu
lazima utatulie kwa njia moja au nyingine ili sisi [Mataifa ya Kiarabu] tuweze
kushughulikia kwa pamoja changamoto nyingi zinazolikumba eneo letu hili," aliongeza.
"Marekani
inalitambua hili na – kama ilivyo kwa Kuwait – inataraji kukomeshwa kwa mzozo
huu ili iweze kuweka nguvu moja kwa moja katika kuzikabili changamoto hizi,"
alisema al-Jarallah.
Wiki hii, Naibu
Waziri wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Ghuba Timothy Lenderking, pamoja
na jenerali wa zamani wa jeshi la wanamaji la Mareni Anthony Zinni, walifanya
ziara maalum katika mataifa ya Kiarabu ambayo iliwapeleka Kuwait, Qatar, Misri,
Saudi Arabia, Bahrain na Oman.
Ziara hiyo
iliripotiwa kuwa na lengo la kutafuta suluhu ya mzozo wa eneo la Ghuba na
kuandaa mazingira ya mkutano wa kilele unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei.
Mwaka jana, Saudi
Arabia na waitifaki wake wanaojumuisha mataifa ya Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain,
kwa pamoja walikata uhusiano na Qatar, wakiituhumu Doha kuwa inaunga mkono
makundi ya kigaidi katika ukanda huo.
Mataifa hayo
yalitishia kuiwekea vikwazo zaidi Qatar iwapo itashindwa kutekeleza masharti
iliyopewa, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kukifunga kituo cha matangazo cha Al
Jazeera chenye makao yake mjini Doha.
Hata hivyo, Qatar
iliyakataa masharti hayo na kukana vikali tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake.
Nayo Kuwait kwa
upande wake imeendelea kutoegemea upande wowote kwenye mzozo huo huku
ikijitahidi kuwa mpatanishi katika mzozo huo.
0 comments:
Post a Comment