Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kenya inajivunia kuwa makazi ya faru wawili tu wa aina yake ambao wamebaki duniani.
Hawa ni faru weupe wa kaskazini au White Northern Rhinos. Faru hawa wanahifadhiwa katika Hifadhi ya Ol Pejeta iliyoko katika eneo la kati ya nchi.
Hawa ni jamii ndogo ya faru weupe, ambao walikuwa wakienea katika maeneo ya Uganda, Chad, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Lakini pia kuna faru weupe wanaoitwa faru weupe wa Kusini au Southern Rhinos. Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha walikuwa 16,801.
Wanaishi katika savanna ya Kenya, Namibia, na Zimbabwe, huku wengi wao wakiwa wanapatikana Afrika Kusini. Faru weupe, licha ya jina lao, lakini sio weupe kwa rangi, wana rangi ya kijivu tu.
Kuitwa "White Rhino" hilo jina "White" inasemekana limechukuliwa kutoka kwa neno la Kiafrikana "weit," linalomaanisha "pana."Ambayo liliashiria midomo yao, ambayo ni mipana na ya mraba ambayo inawasaidia kula nyasi.
Tofauti yao ni ipi?
Hawa faru weupe wa Kusini ni wengi zaidi na ni wakubwa kidogo. Wana manyoya zaidi kuliko wale waliobaki ambao wamehifadhiwa nchini Kenya.
Pembe za faru hawa si pembe kwa maana ya pembe, zao zimeunganishwa kwenye fuvu, zinatoka kwenye ngozi na kuundwa na nyuzi za keratini, sawa na zile zinazopatikana katika nywele na kucha.
Faru mweupe ana mdomo mpana unaomruhusu kula majani ya kijani yanayoota kwenye savanna.
Faru jike mweupe hukomaa wakiwa na umri wa miaka minne au mitano, wakati madume wanaweza kuchukua hadi miaka mitano au zaidi, wanaanza kuzaliana wakiwa na umri wa miaka 10.
Muda wa kubeba ujauzito kwa faru mweupe ni takriban miezi 16.
Faru mweupe ni kati ya wanyama wenye kiwango kikubwa cha ulaji.
Kila siku, hula zaidi ya kilo 50 za nyasi na kuzalisha zaidi ya kilo 20 ya kinyesi, na hivyo kurutubisha udongo.
Kutokana na tabia zao za ulaji wa majani mafupi, faru hawa hawawezi kuishi katika mazingira ya misitu au nyasi ndefu.
Faru weupe hukaa pamoja katika makundi. Madume hulinda himaya zao kwa nguvu kwa kutumia pembe zao na ukubwa wao.
Pia faru hawa, wanapenda maeneo yenye unyevunyevu na tope. Ambapo hujiviringisha na kujifunika, na kuwafunika watoto wao. Hutumia tope kujipoza na kulinda ngozi zao dhidi ya mionzi ya jua na wadudu.
Na wakiwa kati ya wanyama watano wakubwa Afrika, yani Big 5, ni kivutio kikubwa cha utalii. Lakini uwindaji haramu wa pembe zao ni moja ya tishio kubwa kwa faru weupe.
Pembe zao zinahitajika huko Asia, haswa Vietnam na China, kwa matumizi ya dawa za jadi. Wafanyabiashara matajiri hutumia bidhaa za pembe za faru kama njia ya kuonyesha uwezo wao wa pesa.
Takwimu za mwaka wa 2022, zinaonyesha faru 448 waliuawa Afrika Kusini, na 93 huko Namibia.
Nchini Kenya, takwimu rasmi zilionyesha kuwa faru mmoja aliwindwa mwaka 2022.
Kivutio kikubwa ni bei za pembe zao. Biashara ya kimataifa ya pembe za faru imepigwa marufuku na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Viumbe vilivyo Hatarini Kutoweka (CITES), mkataba tangu 1977, hata hivyo, uwindaji wa faru kwa njia haramu bado unaendelea.
Takwimu zaonyesha kuwa kufikia 2022, bei ya pembe za faru katika soko haramu ilifika dola 20,000 kwa kilo kwa pembe za faru wa Afrika. Pembe moja wa faru mweupe inaweza kuwa na uzito wa kilo 4.
Watalamu wanasema ingawa idadi ya faru weupe imeongezeka kwa miaka za hivi karibuni, bado kuna haja ya nchi kuhakikisha kuwa wanatunzwa vizuri ili waendelee kuongezeka.
Wanasema hili litawezekana ikiwa uwindaji wao haramu utaisha kabisa, jambo ambalo bado ni changamoto kubwa.
0 comments:
Post a Comment