Kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani (kulia) na
kiongozi wa Kuwait Sabah al-Ahmad al-Jaber Al Sabah wakihudhuria mkutano wa
Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC) Desemba 6, 2016, mjini Manama.
|
Imeelezwa kuwa Kuwait imeipa Qatar orodha ya masharti
kutoka kwa mataifa ya Ghuba yaliyoiwekea vikwazo Doha katika juhudi za
kuhitimisha mzozo wa kidplomasia ulioligubika eneo la Ghuba.
Mashirika ya habari yamesema kuwa yamepata nakala ya
masharti 13 kutoka kwa moja ya nchi zinazohusika na mgogoro huo. Orodha hiyo
imewasilishwa na Kuwait ambayo imekuwa ikijaribu kutafuta suluhu kati ya pande
mbili zinazozozana.
Kwa mujibu wa orodha hiyo, mataifa hayo yanayoongozwa na
Saudi Arabia yanaitaka Qatar kukifunga kituo chake cha matangazo cha Al Jazeera
chenye makao yake mjini Doha, ikate uhusiano wa kidiplomasia na Iran, ifunge
kambi ya jeshi la Uturuki iliyopo nchini humo na kulipa kiwango cha pesa
ambacho hakijaainishwa kama fidia.
Aidha, Doha imetakiwa kuegemea upande wa mataifa
yanayounda Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba kisiasa, kiuchumi na
kadhalika.
Saudi Arabia na waitifaki wake pia wanaitaka Qatar
kukata mahusiano yote na vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) na
makundi mengine yakiwemo al-Qaeda na Daesh (Dola la Kiislamu).
Qatar imepewa siku 10 kuyatazama masharti hayo na
kuyafanyia kazi.
Maafisa mjini Doha hawajatoa kauli yoyote kuhusu taarifa
hiyo.
Mnamo Juni 5, Saudi Arabia na mataifa kadhaa waitifaki
wake, zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar. Riyadh na washirika wake,
ikiwemo Bahrain, Misri, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), zilikata
mawasiliano yote ya ardhini, baharini na angani dhidi ya Qatar kwa madai kuwa
taifa hilo linafadhili ugaidi na kusababisha changamoto ya kiusalama katika
ukanda mzima, madai ambayo Doha imeyakanusha vikali.
Doha imekaribisha juhudi za usuluhishi kwa lengo la
kuondoa mvutano, lakini ikaweka msimamo kuwa haitaruhusu majirani zake
kuwaamulia masuala mambo yake binafsi na yanayosimamia mamlaka yake kama nchi.
Qatar imesema kuwa haitaingia kwenye mazungumzo mpaka
mataifa hayo ya kiarabu yaondoe kwanza vikwazo dhidi yake.
Hivi karibuni waziri wa Mambo ya Nje, Sheikh Mohammed bin
Abdulrahman Al Thani alisema kuwa nchi yake itayategemea mataifa mengine iwapo
vikwazo hivyo vitaendelea.
Hatua kali dhidi ya Qatar zimekuwa zikilaaniwa na makundi ya
haki za binadamu kama vile shirika la Amnesty International, ambalo lilisema
kuwa mgogoro huo wa kidiplomasia umeyaathiri maisha ya maelfu ya watu.
Kwa sasa mataifa ya Iran na Uturuki yanaipatia Qatar mahitaji ya
chakula huku Uturuki ikiwa imepeleka vikosi vya askari wake kwenye kambi yake
ya kijeshi iliyoko nchini humo.
Mvutano huo uliibuka mwezi jana baada ya Shirika la Habari la
Qatar (QNA) kutoa kauli zilizohusihwa na kiongozi wa taifa hilo Sheikh Tamim
bin Hamad Al Thani, zikiielezea Iran kama “Taifa la Kiislamu lenye nguvu,” kulisifu
vuguvugu la Hamas la nchini Palestina na kumkosoa Rais wa Marekani Donald
Trump.
Baadaye Qatar ilisema kuwa wadukuzi walikuwa wameivamia tovuti
ya QNA na kuchapisha taarifa bandia, lakini kanusho hilo halikuishawishi Riyadh
na waitifaki wake wa Ghuba.
Mapema Jumatano Doha ilitangaza kuwa ina ushahidi kwamba tukio
hilo la udukuzi lilifanywa kutokea moja ya nchi jirani.
UTURUKI YAPINGA KUINGILIWA MAHUSIANO YAKE
Kufuatia kutolewa kwa orodha hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Fikri
Isik, amesema kuwa Ankara haina mpango wa kuondosha kambi yake ya kijeshi ya nchini
Qatar, akaongeza kuwa nchi hiyo inalitazama sharti lolote la kufunga kambi yake
hiyo kuwa ni kuingilia mahusiano yake na Doha.
“Kambi iliyoko Qatar ni ya Uturuki lakini pia inaimarisha
usalama wa Qatar na eneo zima,” Isik alisema katika mahujiano ya kituo cha NTV.
Ankara ilipelekea askari wake nchini Qatar katika hali ya
kuonesha kumuunga mkono mshirika wake kufuatia kuibuka kwa mzozo huo wa
kidiplomasia.
Mnamo mwaka 2014, Uturuki na Qatar zilisaini makubaliano ambayo
yaliruhusu kujengwa kwa kambi ya kijeshi ya Uturuki nchini Qatar. Maafisa wanasema
kuwa askari wasiopungua 3,000 wanaweza kupelekwa nchini humo kama sehemu ya
programu ya Ankara ya kuongeza ushirikiano wa kijeshi na Doha.
0 comments:
Post a Comment