Mwendesha mashitaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu (ICC), Fatou Bensouda ametoa ishara kubwa kuwa mipango ya baadhi ya
nchi za Afrika kutaka kujiondoa kwenye uanachama wa mahakama hiyo haitaathiri
kwa vovyote uchunguzi unaoendelea dhidi ya makosa ya uhalifu wa kivita. Aliapa kuendelea
kuwachunguza wahalifu wanaotenda unyama huo.
Fatou Bensouda amesema kuwa mahakama yake itaendelea na
uchunguzi wake wa awali nchini Burundi ambao ulianza hmwezi Aprili, kwa sababu
anaungwa mkono na zaidi ya nchi 120 wanachana wa mahakama hiyo.
Ghasia ziliibuka nchini Burundi mwezi Aprili mwaka jana
baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania muhula wa tatu madarakani. Ghasia
hizo zimesababisha zaidi ya Warundi laki tatu kukimbia nchi jirani.
Mwezi Oktoba na Novemba mataifa ya Burundi, Afrika
Kusini na Gambia yalitoa taarifa mbele ya Umoja wa Mataifa juu ya kusudio lao
la kujiondoa kwenye mahakama hiyo. Hata hivyo, kujiondoa kwao kutaanza kufanya
kazi rasmi baada ya mwaka mmoja.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika, mataifa hayo
yanaituhumu ICC kuwa ina upendeleo dhidi ya Afrika. Washukiwa 5 waliotiwa
hatiana na mahakama hiyo wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamhuri ya
Afrika ya Kati na Mali.
Lakini ICC imekanusha tuhuma hizo za upendeleo ikisema
kuwa kesi nyingi ziliwasilishwa na serikali zenyewe za Kiafrika.
Waziri huyo wa zamani wa Gambia amenukuliwa na shirika
la habari la Reuters akisema: “Hata kama nchi moja ikiamua kujiondoa ICC, taifa
zima la Afrika linakuwa limerudi nyuma na hilo ni jambo baya kwa bara lote.”
Hata hivyo, ametupilia tuhuma kwamba kesi zote za ICC
zinatoka Afrika akiashiria kuwa mahakama hiyo ina uchunguzi wa kesi 10 za
uhalifu katika mataifa ya Afghanistan, Colombia, Georgia, Iraq, Palestina na
Ukraine.
Wakati kuna wasiwasi wa mataifa mengi kujiondoa kutoka
mahakama hiyo, hasa mataifa ya Afrika, Bensouda amesema kuwa mataifa mengine
wanachama yamesisitiza kushirikiana na mahakama hiyo yenye mamlaka ya
kushughulikia uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya
kimbari.
Urusi ambayo haijawa mwanachama rasmi wa mahakama hiyo
lakini ilisaini Mkataba wa Roma, mwezi huu ilisema kuwa itaondosha saini yake. Ufilipino
nayo inafikiria kuondoa uanachama wake.
Mahakama hiyo iliyoanzishwa Julai 2002, imekuwa kama
kimbilio la mwisho la waathirika ya kivita ambapo huingilia kati pindi mifumo
ya kimahakama ya mataifa wanachama inaposhindwa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu
wa kivita.
0 comments:
Post a Comment