Fidel Castro akizungumza mwezi Julai 2014 alipokutana na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin. |
FIDEL CASTRO WA CUBA AFARIKI DUNIA
Kiongozi mkongwe wa mapinduzi ya Cuba, Fidel Castro, amefariki
dunia akiwa na umri wa miaka 90. Kaka yake, na rais wa sasa wa Cuba ametangaza.
“Amiri jeshi mkuu wa mapinduzi ya Cuba amefariki dunia
saa 4: 29 usiku huu,” Rais Raul Castro ametangaza katika televisheni ya Taifa.
Castro aliendesha vita maarufu vya msituni na kupata
uungaji mkono wa wananchi akafanikiwa kumuondosha madarakani dikteta wa wakati
huo Jenerali Fulgencio Batista mnamo Januari 1, 1959. Baada ya mapanduzi hayo
alitawazwa kama waziri mkuu.
Akiongozi taifa la Kikomunisti, Castro alivunja uhusiano
wa kidiplomasia na taifa la kibepari la Marekani mwaka 1961 na kuzitaifisha
mali za makampuni ya Kimarekani zilizokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni
moja.
Marekani ilianza kuiwekea vikwazo vikali Cuba, ambavyo
ilikabiliana navyo licha ya umasikini kuenea. Uhasama uliendelea – ingawa baadaye
ulikuwa wa maneno tu – kati ya mahasimu hao wawili wa Vita Baridi mpaka Julai 2015,
ambapo mataifa hayo mawili yalianzisha tena uhusiano wa kidiplomasia na
kufungua balozi zao.
Castro aliiongoza Cuba kwa miongo mitano mpaka mwaka
2006 alipokabidhi madaraka kwa muda kwa mdogo wake Raul kwa sababu alitakiwa
kufanyiwa operesheni. Uhamishaji rasmi wa madaraka ulifanyika mwaka 2008.
Wakati wa maisha yake ya kimapinduzi, shirika la Ujasusu
la Marekani, CIA, lilijaribu kumuua mara kadhaa.
Castro mwenyewe anasema kuwa alinusurika majaribio 634
ya kuuawa, mengi yakiratibiwa na CIA au mitandao ya wale waliokuwa uhamishoni
nchini Marekani. Majaribio hayo yanaweza kuwa yalihusisha vidonge vyenye sumu,
siga za sumu, mavazi yaliyotiwa kemikali na vitu vingine.
Castro alizaliwa Agosti 13, 1926 kwa baba mhamiaji wa
Kihispania na mama Mcuba.
0 comments:
Post a Comment