Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard K. Membe (Mb) atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Uturuki
kuanzia tarehe 07 – 09 Mei, 2014 kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa
nchi hiyo, Mhe. Ahmet Davutoglo. Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza na
kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki ambao umedumu kwa kipindi
kirefu sasa.
Aidha, katika ziara hiyo Mhe. Membe na mwenyeji wake
watajadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki
hususan, katika maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mkutano wa Wakuu wa
Nchi wa Afrika na Uturuki uliofanyika mwaka 2008.
Maeneo hayo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo,
mawasiliano, afya, elimu pamoja na amani na usalama.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri ataonana na kufanya
mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Uturuki akiwemo mwenyeji wake, Mhe.
Davutoglo; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri wa Uchukuzi, Usafiri
wa Majini na Mawasiliano, Mhe. Lutfi Elvan; Waziri wa Nishati na Maliasili,
Mhe. Tarrer Yildiz pamoja na kuongea na wafanyabiashara wa Uturuki.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri atafuatana na viongozi
waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Wizara ya
Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Mamlaka ya Majengo
Tanzania na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).
Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment