Maelfu ya waandamanaji nchini Brazil wameweka kambi nje
ya uwanja katika mji wa Sao Paulo kunakotarajiwa kuchezwa mechi ya ufunguzi ya
Mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu.
Waandamanaji hao wanasema kuwa wamechoshwa na ongezeko
la kodi ya nyumba na makazi na wanataka kuonesha hasira zao kwa kitendo cha
nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ilhali suala la umasikini
likiendelea kuwatafuna raia.
Katika mitaa ya Itakera mjini Sao Paulo, watu wapatao 2,000
wametwaa eneo karibu na uwanja wa michezo wa Arena Corinthians, ambao utakuwa
mwenyeji wa mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo yaliyopangwa kuanza mwezi
Juni.
Watu wameonekana wakiendelea kumiminika katika eneo hilo
wakiwa na vifaa vya ujenzi katika hali inayoonekana kuwa wanataka kujenga kambi
ya kudumu na wataendelea kukaa mahali hapo.
Kiongozi wa vuguvugu la watu wasiokuwa na makazi nchini
humo, Laura Cristina da Silva, amesema kuwa wanalazimika kuchagua kati ya
kuwalisha watoto wao na kulipa kodi ya nyumba. Pesa ambayo imetumika kujenga
viwanja vya michezo ingetumika kuwapatia mahala pa kuishi.
Mji wa Sao Paulo ni miongoni mwa miji yenye gharama za
juu kabisa za kodi za pango na makazi duniani.
Wakati hayo yakiendelea, viongozi wa mji huo wanasema
kuwa wameorodhesha maeneo 90 mbalimbali ambayo yanashikiliwa kwa nguvu na watu
wanaodai kuwa hawana mahali pa kuishi.
Kwa miezi kadhaa sasa, hisia za kupinga michuano ya
kombe la dunia nchini humo zimekuwa zikiongezeka. Watu hao wanaikosoa serikali
ya Brazil kuwa pesa iliyotumika kwenye michuano hiyo ingewekezwa katika huduma
bora za afya, elimu, usafiri, makazi na maisha ya watu wenye hali duni za
kimaisha.
Brazil ni nchi kubwa yenye uchumi mkubwa zaidi katika
eneo la Amerika ya Kusini; lakini kwa mujibu wa Benki ya Dunia, asilimia 15.9
ya wananchi milioni 200 wanaishi katika umaskini wa kutupwa.
0 comments:
Post a Comment