Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Dk. Shukuru Kawambwa. |
Ahadi ya serikali
kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kwamba watalipa ada sawa kwa vyuo vyote
nchini kuanzia mwaka ujao wa masomo, imekwama kutekelezeka.
Ahadi ya serikali kupanga viwango sawa vya ada ilitolewa
na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Machi 13, mwaka
huu, wakati akizindua Mfumo wa Muongozo wa Ulipaji wa ada za vyuo vikuu nchini
(SCU).
Waziri Dk. Kawambwa alisema kuwa mfumo huo uliotarajiwa
kuanza mwaka wa masomo wa 2014/15, ulilenga kusaidia wanafunzi, wazazi na
wafadhili kujua ada kwa kozi husika na kusisitiza kwamba vyuo vyote vitatoza
ada sawa.
Aidha, alisema mfumo huo utaongeza ufanisi wa utoaji
mikopo kwa wanafunzi kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB).
Alifafanua kwa wapo kwenye mchakato wa kuja na mfumo kwa
ajili ya shule za msingi na sekondari.
Uwezekano wa kutotekelezeka kwa mfumo wa gharama sawa
katika vyuo vya elimu ya juu ulielezwa jana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU) kwamba ada za vyuo vya elimu ya juu hazitaweza kuwa sawa kutokana na tofauti ya miundombinu
pamoja na gharama za uendeshaji miongoni mwa vyuo hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Magishi Nkwabi Mgasa, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu SCU.
Prof. Mgasa alisema kuwa gharama za ada haziwezi kuwa
sawa kwa kuwa kuna vyuo ambavyo vilianzishwa kwa ajili ya biashara na
vilivyoanzishwa kwa ajili ya huduma hususani ambavyo vinamilikiwa na serikali.
Profesa Mgasa aliongeza kuwa vilevile, kuna tofauti ya
hadhi ya vyuo hivyo kwani vingine vina vifaa vya kisasa zaidi ikiwa ni pamoja
na majengo, maabara na madarasa, wakati vingine havina ikiwamo walimu bora
wenye viwango vya juu vya elimu na uzoefu.
Kutokana na tofauti hizo, alisema haitawezekana vyuo
vyote vya elimu ya juu kuwa na ada inayolingana.
Hata hivyo, alisema mfumo huo wa gharama elezeki utaanza
kutumika mwaka ujao wa masomo, lakini TCU itahakikisha hakuna tofauti kubwa ya
ada.
Profesa Mgasa alibainisha kwamba mfumo huo utasaidia
katika kupunguza malalamiko kutoka kwa wadau wa elimu kuhusu gharama za ada kwa
elimu ya juu nchini.
“Suala la kuamua gharama za ada za masomo ya elimu ya
juu limekuwa ni mjadala wa moto na wa muda mrefu nchini, na majaribio mengi
yameshafanywa na serikali kuanzia mwaka 2000,” alisema na kuongeza:
“Kutokuwa na mwongozo wa gharama, kumesababisha taasisi
za elimu kutumia njia nyingine ambazo zimeleta mkanganyiko, malumbano miongoni
mwa wadau, wazazi na jamii kwa ujumla wake,” alisema Prof. Mgasa.
Kwa sasa Tanzania ina vyuo vikuu 52. Kati ya hivyo, 33
ni vyuo vikuu kamili wakati 19 ni vyuo vikuu vishiriki.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment