Nahodha wa klabu ya Arsenal Thomas Vermaelen, amemtaka
meneja wa klabu hiyo Arsene Wenger kusaini mkataba mpya wa kuendelea kukinoa
kikosi cha klabu hiyo.
Thomas Vermaelen, amemtaka Arsene Wenger, kufanya hivyo kufuatia
taarifa kueleza wazi kwamba babu huyo mwenye umri wa miaka 64, bado hajafanya
maamuzi ya kusaini mkataba mpya licha ya viongozi wa ngazi juu kuuwasilisha
mkataba huo mezani kwake tangu majuma mawili yaliyopita.
Vermaelen, amesema itakua ni faraja kwake kumuona Arsene
Wenger, akiendelea kuinoa klabu hiyo ambayo bado inahitaji mchango wake licha
ya kukabiliwa na changamoto ya kusaka taji kwa zaidi ya miaka saba iliyopita.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 28 amesema tangu
aliposajiliwa klabuni hapo amekua na maisha mazuri na meneja huyo kutoka nchini
Ufaransa, kutokana na hulka aliyonayo ya kuishi na vizuri na wachezaji.
"Kila mmoja anataka Arsene wenger aendelee kubaki kwa
kipindi kingine kirefu kijacho, ni shujaa kwetu na kila mmoja klabuni hapa
amekua akimuona kama jemedari ambae siku zote anataka kuona jeshi lake
halitetereki, licha ya mafanikio ya mataji kuchelewa " Varmaelen
aliliambia gazeti la Daily Mirror
"Utamaduni wa ufundishaji wake ni wa kipekee ambao
sijawahi kuuona kwa meneja mwingine, hivyo halitokua jambo la kupendeza
miongoni mwetu kama ataacha kusaini mkataba mpya na kukubali kuondoka mwishoni
mwa msimu huu. Aliongeza beki huyo aliyesajili na klabu ya Arsenal akitokea
kwenye klabu ya Ajax Amsterdam ya nchini Uholanzi mwaka 2009.
Arsene Wenger mwenye umri wa miaka 64, amekua na maamuzi
magumu ya kukubali kusaini mkataba mpya tangu kikosi chake kiliposhindwa kumpa
faraja wakati alipotimiza mchezo wa 1000 tangu alipojiunga na klabu ya Arsenal
mwaka 1996, ambapo The Gunners katika mchezo huo walikubali kufungwa mabao sita
kwa sifuri dhidi ya Chelsea.
0 comments:
Post a Comment