Meneja wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho amekanusha taarifa
za kutokua na maelewano mazuri na mshambuliaji kutoka nchini Sweden pamoja na
klabu ya Paris St German ya nchini Ufaransa, Zlatan Ibrahimovic.
Jose Mourinho amekanusha taarifa hizo baada ya kuulizwa na
waandishi wa habari katika mkutano maalum ambao ulikua unazungumzia maandalizi
ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya robo fainali ambapo usiku
wa hii leo Chelsea watakua jijini Paris wakijaribu kutengeneza mazingira ya
kuandaa njia ya kupenya na kuelekea katika hatua ya nusu fainali dhidi ya PSG.
Jose Mourinho, amesema hakuwahi kuwa na ugomvi na
mshambuliaji huyo kama inavyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari ambapo
inaelezwa wawili hao walikorofishana wakati wakiwa kwenye klabu ya Inter Milan
ya nchini Italia.
Mourinho, amesema mengi yalizungumzwa juu ya mahusiano kati
yake na Zlatan Ibrahimovic, ambapo baadhi ya waandishi wa habari walidai yeye
kama meneja alikuwa chanzo cha mshambuliaji huyo kuondoka Inter Milan na
kujiunga na FC Barcelona, kitu ambacho amekipinga.
Wakati huo huo mshambuliaji kutoka nchini Sweden Zlatan
Ibrahimovic ameonyesha kuridhishwa na maisha anayoishi huko jijini Paris baada
ya kusajiliwa na klabu tajiri jijini humo PSG mwaka 2012 akitokea AC Milan ya
nchini Italia.
Zlatan Ibrahimovic, ameonyesha kuridhishwa na maisha ya
jijini humo kwa kusema huenda ikawa vigumu kwake kuamua kuondoka kwenye klabu
hiyo siku za usoni licha ya kuhusishwa na mipango ya kutaka kumalizia soka lake
nchini Uingereza.
Amesema bado hajafanya maamuzi sahihi ya kufikiria ni wapi
atakapomalizia soka lake, lakini ukweli ni kwamba anaendelea kufurahishwa na
mwenendo mzuri wa klabu yake ya PSG ambayo imedhamiria kuleta mapinduzi ya soka
barani Ulaya.
Chelsea wanajiandaa kucheza mchezo wa ligi ya mabingwa
barani Ulaya hatua ya robo fainali dhidi ya PSG baada ya kuwachomoa kwenye
michuano hiyo mabingwa wa soka wa nchini Uturuki Galatasaray, ili hali matajiri
wa jijini Paris walifanikiwa kuingia katika hatua hiyo kwa kuwafunga Schalke 04.
0 comments:
Post a Comment