Kwa uchache watu watano wamepoteza maisha na wengine kadhaa
kujeruhiwa vibaya sana nchini Chile katika tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.2
kwa kipimo cha Richta katika eneo la kaskazini la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Rodrigo
Penailillo, wanaume wanne na mwanamke mmoja walipatwa na kadhia hiyo katika
miji ya Iquique na Alto Hospicio.
Wizara hiyo imesema kuwa watu hao walikufa kutokana na
mshituko wa moyo au kuangukiwa na vifusi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa tetemeko hilo lilikuwa kwenye
kina cha kilometa 20.1 (maili 12.5), umbali wa kilometa 95 (maili 59) kaskazini
magharibi mwa mji wa Iquique kwenye pwani ya kaskazini ya nchi hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Chile, Michelle Bachelet, ameyatangaza
maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo kuwa kanda ya maalumu ya majanga. Rais huyo
alitarajiwa kusafiri kwenye mikoa ya Arica na Tarapaca.
Kufuatia tetemeko hilo, Kituo cha Tahadhari ya Tsunami kwenye
eneo la Pacific kilitoa tahadhari kwa eneo zima la pwani ya Pacific ya Amerika
ya Kusini.
Idadi kadhaa ya barabara nchini humo ziliripotiwa kufungwa
kutokana na maporomoko ya ardhi. Tetemeko hilo pia lilisababisha umeme
kukatika.
Maelfu ya raia wa nchi hiyo wanaoishi katika maeneo ya pwani
wameagizwa kuyahama makazi yao.
Katika siku za hivi karibuni, maeneo ya kaskazini mwa nchi
hiyo yamekuwa yakishuhudia matetemeko ya ardhi.
Mnamo Machi 30, tetemeko la ukubwa wa 6.0 liliyakumba maeneo
ya pwani ya Pacific ya nchi hiyo, likifuatiwa na matetemeko madogo mawili.
Chile ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya
matetemeko ya ardhi duniani.
0 comments:
Post a Comment