Shirikisho la soka nchini Ureno, limekamilisha mpango wa kusaini
mkataba mpya na kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Paulo Jorge Gomes Bento, ambae kwa
sasa anatafakari namna ya kukisaidia kikosi chake kwa ajili ya fainali za kombe
la dunia za mwaka 2014.
Shirikisho la soka nchini Ureno limekamilisha mpango huo
baada ya kufanya mazungumzo na kocha Bento ambapo iliionekana kuna haja ya
pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi kwa pamoja.
Sababu kubwa ambayo ilifanya mazungumzo ya pande hizo mbili
kuanzishwa mwanzoni mwa mwaka huu, ni hatua ya timu ya taifa ya Ureno kufaulu
kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka huu ambazo zitafanyika nchini
Brazil, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Sweden mabao manne kwa mawili katika
mchezo wa hatua ya mtoano ukanda wa barani Ulaya mwaka jana.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44, ambae alichukua jukumu
la kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Ureno mwaka 2010, akichukua nafasi ya
Carlos Queiroz, amekubalia kusaini mkataba wa miaka miwili ambao utamuweka
madarakani hadi mwaka 2016.
Bento amesema hatua ya kusaini mkataba mpya imempa nafasi
ya kuamini bado mchango wake unahitajika katika harakati za kuisaidia timu ya
taifa ya Ureno, ambayo katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu
zitakazochezwa nchini Brazil imedhamiria kufika mbali tofauti na katika fainali
zilizopita.
“Sina budi kufanya kinachokusidiwa na kila mmoja anaeipenda
timu ya taifa ya Ureno, na nitahakikisha ninafanya kazi yangu kwa uadilifu
mkubwa kwa kusaidiana na watu wangu wa karibu kwa lengo la kukabiliana na
changamoto zilizo mbele yetu” Amesema Paulo Bento.
“Najua nina kibarua kingine mara baada ya fainali za kombe
la dunia za mwaka 2014, nitatakiwa kuipeleka Ureno katika fainali za mataifa ya
barani Ulaya za mwaka 2016, hivyo sio kazi ndogo kwangu” Amesisitiza Bento
ambae aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Ureno kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka
2002.
Kabla ya kuifikisha timu ya taifa ya Ureno kwenye fainali
za kombe la dunia za mwaka 2014, Paulo Bento aliifikisha timu hiyo kwenye hatua
ya nusu fainali katika michuano ya barani Ulaya ya mwaka 2012, kabla ya
kutolewa kwa mikwaju ya penati na mabingwa wa soka barani humo timu ya taifa ya
Hispania.
Katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, timu ya
taifa ya Ureno imepangwa katika kundi la saba sambamba na timu ya taifa ya
Marekani, Ghana pamoja na Ujerumani.
0 comments:
Post a Comment