MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa
tahadhari ya kuwepo vipindi vya mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini
kwa siku nne mfululizo.
Taarifa iliyotolewa jana na
Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi ilisema kiwango cha uhakika wa kuwapo kwa
matukio hayo ni kwa asilimia 70.
Alisema matukio hayo yameanza Aprili
11, mwaka huu na yataendelea hadi 14 mwaka huu.
Alisema kutakuwepo na vipindi vya
mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24, upepo mkali unaozidi kilometa
40 kwa saa na mawimbi makubwa, yanayofikia mita mbili katika ukanda wa pwani.
Alitaja maeneo yanayotarajia
kuathirika kuwa ni Visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Tanga. Kuna uwezekano mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro nayo itaathirika na
hali hiyo.
Dk Kijazi alisema hali hiyo,
inatokana na kuimarika zaidi kwa ukanda wa mvua wa ‘Inter-tropical Convergence
Zone (ITCZ)’, ambao umeambatana na ongezeko la unyevunyevu katika eneo la
Bahari ya Hindi.
Alionya wakazi wa maeneo hatarishi,
watumiaji wa bahari na mamlaka zinazohusika na maafa, kuchukua tahadhari
zinazotakiwa, kutokana na hali hiyo. Alisema kwamba mamlaka hiyo inaendelea
kufuatilia hali hiyo na itatoa taarifa kila itakapobidi.
0 comments:
Post a Comment