Mchumi aliyebobea Profesa Ibrahimu Lipumba, amepinga
kauli za kuwa Serikali tatu ina gharama na badala yake akasema wanaopendekeza
hizo hawana nia njema na Tanzania.
Hata hivyo, alitoa pendekezo ndani ya Bunge kuwa hakuna
haja ya kuendelea kujadili rasimu nzima ya katiba kwani kukataa Serikali tatu
ni sawa na kuipinga rasimu yote ambayo imeundwa kwa mfumo wa Serikali tatu.
Profesa Lipumba ambaye ni Mjumbe wa bunge la Katiba,
alitoa kauli hiyo juzi aliposimama kutoa maoni ya wajumbe wachache katika
kamati namba tisa ambapo alionyesha shaka ya uwezo wa kufikiri wa wajumbe wengi
wanaopinga maoni ya wananchi kuhusu Serikali tatu.
Hoja za Lipumba zilionekana kuvuta zaidi hisia za
wajumbe na kushangilia ndani na nje ya ukumbi wa bunge kitendo kilichoonekana
kuwakera wajumbe ambao ni kundi la wengi.
“Kupendekeza Serikali mbili ni sawa na kuvuruga na
kuwabeza wananchi katika maoni yao, sasa kuna haja gani ya kuendelea kujadili
vitu hivyo kama si kupoteza muda wa bure hapa,”alisema Lipumba.
Alitolea mfano wa wasomi wengi ambao wakati wote
wamekuwa wakipendekeza mfumo wa Serikali tatu, lakini cha ajabu wakiingia
bungeni wanapinga jambo ambalo alisema lazima washtakiwe kwa wananchi.
Lipumba alisema wakati wa tume ya Warioba, hata Ofisi ya
Waziri Mkuu ilipendekeza mfumo wa Serikali tatu lakini akasikitishwa ndani ya
kamati yao bado viongozi wengine kutoka katika ofisi hiyo wamepinga.
“Haya ni mambo ya ajabu sana, hivi nani kawashughulikia
huko, mbona awali ofisi ya Waziri Mkuu ilikubali serikali tatu leo mnapinga ina
maana mnampinga kiongozi wenu,” alihoji Lipumba na kuongeza.
“Hata nyinyi wajumbe kutoka Baraza la Wawakilishi, kule
Zanzibar mlitoa maoni ya kuunga mkono Serikali tatu leo hii mnakataa, sasa
niwaulize hivi mnaweza kuthubutu kusimama pale Kibandamaiti na kuzungumzia
Serikali mbili, nani atawaelewa.”
Alisema wanaosema Serikali tatu zina gharama ni wale
ambao wanataka rasilimali za Tanzania ziendelee kutafunwa na wachache kwa
kupora kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati wote.
Alitolewa mfano kuwa fedha nyingi zinazotengwa na bunge
hazifanyi kazi iliyokusudiwa na badala yake zinaishia mikononi mwa wajanja
wachache ambao ndio wanaopigania suala la muundo wa serikali mbili.
Alizitaja Wizara Mambo ya Nje kuwa katika bajeti
iliyopitishwa na bunge mwaka jana, matumizi yake yalizidi hadi kufikia asilimia
146, Wizara ya Tamisemi asilimia 240 na Ulinzi zaidi ya asilimia 160.
“Hapo ndipo tunapolalamikia, miradi mingi ya wananchi
fedha haziendi huko wananchi wanalia wakati kuna maeneo ambayo yanatumia ovyo
pesa za walipa kodi bila ya utaratibu, tunataka katiba yenye meno hii
imeshindwa kwa muda wote wa miaka 50 na haitaweza tena.”
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment