Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra |
Waziri Mkuu wa
Thailand, Yingluck Shinawatra amekataa kujiuzulu kwa madai kuwa wito unaotolewa
na waandamanaji wa kumtaka kufanya hivyo sio wa kikatiba.
“Ninaweza kufanya
chochote kwa ajili ya kuwafurahisha wananchi wangu, nina utashi wa kufanya
hivyo, lakini kama waziri mkuu, kila ninachokifanya lazima kiwe ndani ya
katiba,” amesema waziri mkuu huyo katika hotuba yake kwa taifa lake.
Jana kiongozi wa
upinzani, Suthep Thaugsuban, alitoa muda wa mwisho wa siku mbili kwa bibi Yingluck
ajiuzulu na “kuyarejesha madaraka kwa wananchi.”
Waziri Mkuu alijibu na
kusema kuwa takwa la kuhamisha madaraka kutoka kwa waziri mkuu aliyechaguliwa
kidemokrasia na kuyahamishia kwa wananchi “halipo chini ya sheria ya katiba.”
Waandamanaji nchini
humo wanaipinga serikali ya Yingluck Shinawatra, ambaye ni dada wa waziri mkuu
wa zamani Thaksin Shinawatra
aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi ya mwaka 2006. Thaksin, ambaye
anadaiwa kuwa na mkono wa nyuma ya pazia kwenye serikali ya sasa, amekuwa
akiishi uhamishoni tangu alipong’olewa madarakani.
Aidha, Yingluck alieleza
kuwa jeshi la nchi hiyo halitaegemea upande wowote na anajua vyema kwambwa
wanataka kuona nchi ikiwa katika amani.
Kwa mara nyingine, polisi
wamekabiliana na waandamanaji hao wanaoipinga serikali, ambao wanajaribu kuyazingira
na kuyakalia majengo ya serikali ikiwemo ofisi za Baraza la Mawaziri la nchi
hiyo lililopo mjini Bangkok. Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi, risasi za
mpira na maji ya kuwasha katika kuwatawanya.
Waandamanaji hao
wameshayashikilia majengo kadhaa ya serikali ikiwemo jengo la wizara ya fedha.
Kiasi cha askari 3,000 wa
usalama wamewekwa kwenye ofisi muhimu za serikali.
Maandamanaji hayo
yalishtadi mwishoni mwa juma baada ya waandamanaji wanaoiunga mkono serikali,
wanaojulikana kama “fulana nyekundu”, walipofanya maandamano kuonesha uungaji
mkono kwa serikali ya bibi Yingluck.
Ripoti zinasema kuwa
watu kadhaa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika maandamano ya hivi
karibuni yaliyoutikisa mji mkuu, Bangkok.
Viongozi wa maandamano
wanatoa wito wa kufanyika kwa mgomo wa nchi nzima katika jaribio la kuishinikiza
serikali kujiuzulu.
Maandamano nchini humo
yaliibuka pale bunge la seneti lilipoukataa muswada wa serikali ambao ungetoa
msamaha kwa waziri mkuu aliyetimulia, Thaksin Shinawatra na kumuwezesha kutoka
uhamishoni na kurejea nchini.
0 comments:
Post a Comment