MASHITAKA 11 dhidi ya
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, yamebainisha kuwa kosa
kubwa la kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya kutaka kuwania nafasi ya
Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Chanzo chetu cha habari
kilichoona mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa washitakiwa, kimebainisha kuwa
makosa saba kati ya makosa 11, yanahusu kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu
Mwenyekiti wa Taifa.
“Ukiona hayo mashitaka
yenyewe ndugu yangu, yanajirudia rudia na kuzunguka katika kosa moja la nia ya kuwania
nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa… angalia kosa la kwanza, kosa la tatu, tano, sita
nane na tisa, ni kama vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.
“Hata hivyo kwa jinsi
mgawanyiko ulivyo ndani ya chama sasa, nakuhakikishia hawa jamaa (Zitto, Dk
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba), watarudishwa katika nyadhifa zao na hakuna
atakayeadhibiwa,” alisema mtoa taarifa wetu.
Alinukuu kauli ya
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu aliyehoji kama makosa
wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi cha kuyeyusha mema aliyoyafanya
katika chama. “Si umesikia akina Baregu wakizungumza? Kwa mashitaka yale
nakuhakikishia kitakachofanyika ni kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema
mtoa habari wetu.
Kosa la
kwanza kwa Zitto,
Dk Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya Chama inayokataza kukashifu
chama, kiongozi au mwanachama yeyote. Katika maelezo ya kosa hilo, akina Zitto
wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa
na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
Moja ya madai katika
mashitaka hayo, ni kilichoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe
amekuwa akinunua vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe
na ambayo haihojiwi popote. Wanadaiwa pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni
mdhaifu kwa kumruhusu Mbowe kuingilia shughuli za kiutendaji.
Zitto na wenzake
wanadaiwa katika kosa la pili,
kutokuwa wawazi na wa kweli wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu
na udanganyifu kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII.
Katika kosa
la tatu, wanadaiwa kutoa
tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao halali na utaratibu wa ngazi
zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).
Katika kosa
la nne, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya
ukabila, udini au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama,
miongoni mwa jamii, kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo wanadaiwa kwenda
kinyume na kipengele cha 10.1 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Akina Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya
kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa chama au wanachama, kinyume na
kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Katika kosa la sita ambalo mtoa habari wetu alisema ndio
kubwa, Zitto na wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea
uenyekiti wa Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi hiyo.
Hatua hiyo inadaiwa
kuwa ni kinyume na kifungu 2.C cha Muongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania
Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na Serikali wa 2012.
Zitto na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa kutengeneza mitandao ya
kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikishia ushindi kinyume na
kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika kosa
la nane, Zitto na wenzake
wanadaiwa kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka
kugombea nafasi ya uenyekiti kinyume na kifungu 2 (E) cha Muongozo wa Kuwania
Uongozi.
Katika kosa hilo,
kumewekwa maelezo ya ziada kuwa kosa hilo linaunganishwa na kosa la kwanza
ambalo washitakiwa wanadiwa kuwakashifu Mbowe, Dk Slaa na Lema.
Kosa la
tisa, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na upinzani
dhidi ya chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama
wakati wa uchaguzi wa chama, kinyume na kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za
Uendeshaji.
Kosa la
kumi linamhusu Zitto peke yake, ambapo anaidaiwa
kukashifu chama na kiongozi wa chama nje ya Bunge kinyume na kifungu 2 C (B),
kikisomwa pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.
Katika hilo Zitto kwa
kushirikiana na baadhi ya viongozi wa chama yaani Dk Mkumbo na Mwigamba na mtu
mwingine ambaye hajajulikana, wanadaiwa kusambaza waraka uitwao Mkakati wa
Mabadiliko 2013.
Mkakati huo, unadaiwa
kukashifu chama na/ au viongozi wake wakuu kama ilivyoelezwa katika kosa la
kwanza, tatu, nne na nane.
Mwisho
katika kosa la 11, Zitto na wenzake wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya
chama kinyume na kanuni ya 3 F ya Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Bunge.
CHANZO: HabariLeo

0 comments:
Post a Comment