Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, amesema
kuwa amewasilisha barua yake ya kujiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu na
uenyekiti wa muungano wa vyama vinavyotawala nchini humo.
Tangazo la Hailemariam linakuja huku kukiwa na mzozo wa
kisiasa na ghasia katika taifa hilo la pembe ya Afrika, ambalo limeshuhudiwa
kuachiwa huru kwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa ili kutuliza hali ya mambo.
"Ukosefu wa utulivu na mzozo wa kisiasa
vimesababisha kupotea kwa maisha ya watu na wengi kukosa makazi," alisema Hailemariam
katika hotuba yake iliyotangazwa kwa njia ya televisheni.
"Suala la kujiuzulu naliona kama hatua muhimu ya
kuendeleza mageuzi yatakayopelekea kuwepo kwa amani thabiti na demokrasia,"
alisema.
Hata hivyo, Hailemariam aliongeza kuwa ataendelea
kushikilia wadhifa huo kwa muda mpaka waraka wake wa kujiuzulu utakapokubaliwa
na chama tawala nchini humo, EPRDF, na bunge la taifa hilo.
Bunge la nchi huyo linatarajiwa kukutana siku ya Ijumaa
kumchagua mrithi wa Hailemariam na inatarajiwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa
nchi hiyo, Workneh Gebeyehu,
atachaguliwa kuchukua nafasi hiyo.
Mamia ya watu wamepoteza maisha katika wimbi la ghasia
nchini kote ambazo awali zilichochewa na mpango wa maendelea ya mji mkuu, Addis
Ababa, mwaka 2015.
Ghasia zilisambaa baada ya maandamano dhidi ya uminywaji
wa uhuru wa kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu yalipoibuka.
WAFUNGWA
WAACHIWA HURU
Maandamano ya kudai uhuru zaidi yalianza mwaka 2015 na
kuenea sana katika mikoa ya Oromia na Amhara, ambayo ni maeneo yenye wakazi
wengi zaidi, kabla ya kusambaa kwenye maeneo mengine ya nchi hiyo.
Ghasia hizo zilipelekea kutangazwa kwa hali ya dharura
iliyodumu kwa miezi kadhaa.
Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikituhumiwa kuwakamata
waandishi wa habari wanaoikosoa serikali na viongozi wa upinzani.
Mashirika ya haki za binadamu na makundi ya upinzani
yamekuwa yakitoa wito wa kuachiwa huru kwa wakosoaji hao, yakisema kuwa
wamekamatwa kwa tuhuma za kutungwa na kwamba wanaadhibiwa kwa sababu ya maoni
yao.
Mnamo mwezi Januari, Hailemariam alitangaza kuwa
serikali yake ingewaachia huru wafungwa hao na mpaka sasa wafungwa wapatao 7,000
wameondolewa mashitaka au kusamehewa.
Kiongozi huyo mwanataaluma aliyegeukia siasa ameiongoza
Ethiopia tangu mwaka 2012, baada ya kifo cha kiongozi wa zamani Meles Zenawi.
Wakati wa utawala wa Meles alihudumu kama naibu waziri
mkuu na waziri wa mambo ya kigeni kabla ya wadhifa huo, na pia alichaguliwa
kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka 2013.
0 comments:
Post a Comment