Rais wa zamani wa Brazil Luiz Lula da Silva |
Kiongozi wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye
ni mshindani mkuu anayewania kushinda katika uchaguzi wa mwakani wa kiti cha
urais, amekutwa na hatia ya ufisadi na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka tisa na nusu jela.
Hukumu hiyo ni anguko kubwa kwa Lula, ambaye ni mmoja wa
wanasiasa maarufu sana nchini humo, na ni pigo dhidi ya azma yake ya kurudi
kwenye ulingo wa siasa. Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha wafanyakazi, ambaye
alisifiwa sana kimataifa kwa sera zake za kupunguza ukosefu wa usawa nchini
mwake, anakabiliwa na kesi nyingine nne za ufisadi na mustakbali wake
unategemea rufaa atakayoikata.
Hukumu hiyo ni ya aina yake dhidi ya kiongozi aliyewahi
kushika wadhifa wa juu kabisa ambayo uchunguzi wake ulidumu kwa zaidi ya miaka
3 na kufichua mfumo wa rushwa ya kiwango cha juu kati ya wafanyabiashara na
serikali.
Jaji Sergio Moro alimtia hatiani Lula mwenye umri wa miaka
71 kwa kosa la kupokea reais milioni 3.7 (sawa na dola milioni 1.2) ambayo ni
rushwa kutoka kampuni ya uhandisi ya OAS SA, kiwango ambacho waendesha
mashitaka walisema kuwa kampuni hiyo ilikitumia kumjengea Lula nyumba ya
ufukweni ili aisaidie kushinda zabuni za mikataba na kampuni ya mafuta ya
serikali ya Petroleo Brasileiro.
Mawakili wa serikali wamemtuhumu Lula, ambaye ni rais wa
kwanza wan chi hiyo kutoka jamii ya wafanyakazi kuanzia mwaka 2003 mpaka 2011, kwamba
alisanifu mpango wa ufisadi wa muda mrefu ambao uligunduliwa katika uchunguzi
maarufu wa kampuni ya Petrobras.
Jopo la wanasheria wa Lula lilisema katika taarifa yake
ya mtandaoni kuwa hana hatia na kwamba watakata rufaa.
"Kwa zaidi ya miaka mitatu, Lula amekuwa mhanga wa
uchunguzi ulichochewa kisiasa," waliandika. “Hakuna ushahidi wa kuaminika
uliotolewa kumuweka hatiani, na ushahidi lukuki wa kuthibtisha kuwa hana hatia
ulipuuzwa."
Wakili wa Lula, Cristiano Martins, amemtuhumu mara kwa
mara jaji Moro kwamba ana upendeleo dhidi ya mteja wake, tuhuma ambazo Moro
amezikanusha vikali.
Moro alieleza katika hukumu yake kuwa hakutumia hisia
zake binafsi kutoa hukumu, tofauti kabisa na tuhuma alizoelekezewa.
"Ni jambo la kuhuzunisha kwamba rais wa jamhuri
anahukumiwa kwa kufanya uhalifu,” Moro alisema. “Hata uwe na cheo gani, hakuna
aliye juu ya sharia.”
Sarafu ya Brazil iliimarika kufuatia uamuzi huo na
kufikia kiwango chake cha juu kabisa ndani ya miezi miwili. Orodha ya soko la
hisa imepanda kwa kiwango kikubwa. Wawekezaji wana wasiwasi kwamba utawala
mwingine wa Lula unamaanisha kurejea kwa sera za uchumi unaohodhiwa zaidi na
serikali na sera ambazo sio rafiki kwa biashara.
"PIGO KWA SIASA ZA MRENGO WA KUSHOTO"
Iwapo mahakama ya rufaa itakubaliana na hukumu hiyo,
basi Lula hatoruhusiwa kushika wadhifa wa umma, rufaa ambayo inatarajiwa
kuchukua angalau miezi 8 kabla ya hukumu.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa asipogombea, chama cha
mrengo wa kushoto nchini humo kitakuwa katika wakati mgumu sana kwa kulazimika
kujijenga upya na angalau kutafuta kiongozi atakayeweza kuibuka na kujitoka
kwenye kivuli ambacho Lula amekiweka kwenye siasa za nchi hiyo kwa miongo
mitatu.
"Kukosekana kwa Lula kunaibua shimo katika medani
za kisiasa na kutengeneza ombwe kubwa la uongozi kwa chama cha mrengo wa
kushoto," alisema Claudio Couto ambaye ni mwanasayansi wa siasa kutoka
Chuo Kikuu cha Getulio Vargas Foundation. "Sasa hivi tumeingia katika hali
ya mvutano mkubwa wa kisiasa ambao ni zaidi ya ghasia ambazo tulikuwa nazo
mwaka jana.”
Couto anasema kuwa anatarajia mahakama ya rufaa
itapitisha hukumu hiyo. Iwapo itakuwa hivyo basi itakifanya kinyang’anyiro cha
urais mwaka 2018 kuwa wazi na kuibuka uwezekano wa mgombea mgeni kwenye ulingo
wa siasa kuibua mshindi, hasa ikichukuliwa kwamba wagombea wengi nao wanazungukwa
na wingu la uchunguzi dhidi ya ufisadi.
MAMBO KWENDA MRAMA?
Awamu mbili za utawala wa Lula zilikuwa maarufu kwa
ustawi wa bidhaa na hivyo kuufanya uchumi wa Brazil kwa muda kuwa miongoni mwa
uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi ulimwneguni. Sera zake za mambo ya nje,
kuiunganisha Brazil na mataifa mengine makubwa yanayoendelea, kuliinua nchi
hiyo kwenye jukwaa kubwa la kimataifa.
Katika hali ya kutaka kupanda chati zaidi, Lula alipuuza
ushawishi wake wa kiuchumi na kisiasa kwenye ukanda wa kaskazini na kuanza
kujihusisha katika matatizo ya kimataifa, kama vile suala la amani ya Mashariki
ya Kati na kujiingiza kwenye kadhia ya programu ya nyuklia ya Iran.
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, wakati fulani
alimuelezea kama mwanasiasa mashuhuri zaidi duniani.
Baada ya kuondoka ofisini na kufanikiwa kumuweka
madarakani mrithi wake aliyemteua mwenyewe, Dilma Rousseff, uchumi wa Brazil
ulitetereka, ambapo sasa taifa hilo linaanza kutoka kwenye mdororo mbaya zaidi
kuwahi kuikumba.
Rousseff aliondolewa madarakani kwa kura ya bunge mwaka
jana kutokana na kukiuka taratibu za kibajeti. Yeye na wafuasi wake wanasema
kuwa kuondolewa kwake yalikuwa ‘mapinduzi’ yaliyoratibiwa na makamu wake ambaye
kwa sasa ni rais wa nchi hiyo, Michel Temer, ambaye yeye mwenyewe anakabiliwa
na tuhuma za ufisadi.
Wakati wa kesi yake, Lula alitoa utetezi mkali uliodumu
kwa muda wa saa tano akidai kuwa hana hatia na kwamba kesi hiyo ilichochewa
kisiasa na sio matumizi mabaya ya fedha za umma.
"Lakini kinachotokea sasa hakitanikatisha tamaa,
badala yake kitanipa hamasa ya kujitokeza na kusema zaidi," Lula alisema
katika ushahidi wake. “Nitaendelea kupambana."
0 comments:
Post a Comment