Mlipuko wa bomu umeua watu wasiopungua 52 ndani ya
hospitali kuu katika mji wa Quetta kusini magharibi mwa Pakistan.
Mlipuko huo uliotokea leo katika wodi ya dharura, umethibitishwa
na Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Balochistan, Sarfaraz Bugti.
Makumi ya watu wamejeruhiwa katika tukio hilo ambalo
limetokea wakati kundi la mawakili lilipokuwa limekusanyika ndani ya hospitali
hiyo kwa ajili ya kufuatilia mwili wa mwanasheria maarufu ambaye alikuwa
amepigwa risasi asubuhi ya leo.
Bilal Anwar Kasi, ambaye alikuwa rais wa zamani wa Chama
cha Mawakili wa Balochistan, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye silaha
mjini humo.
Ripoti zinasema kuwa milio ya risasi ilisikika baada ya
polisi kuizingira hospitali hiyo na kulifunga eneo hilo baada ya mlipuko.
Bugti amelaumu “ulegevu wa usalama” akisema kuwa yeye
mwenyewe analichunguza tukio hilo. Amesema kuwa ni mapema sana kung’amua kundi
lipi au mtu gani ambaye amehusika na shambulizi hilo.
Balochistan imekuwa ikishuhudia ghasia za kikabila na
mashambulizi mengi kwa miaka kadhaa, huku jamii ya Hazara katika jimbo hilo
ikilengwa mara kwa mara na matukio ya utekaji na mauaji yanayofanywa na
wanamgambo wenye siasa kali.
Jimbo hilo lenye umasikini mkubwa licha ya kuwa na
rasilimali za gesi na madini, linapakana na nchi jirani ya Afghanistan kwa
upande wa kaskazini na Iran kwa upande wa mashariki.
Shambulizi baya kabisa dhidi ya jamii ya Hazara
lilitokea mwaka 2013, ambapo zaidi ya watu 180 wa jamii hiyo waliuawa katika
milipuko miwili mjini Quetta.
Maelfu ya watu wameuawa ndani ya muongo mmoja kutokana
na wimbi la ghasia lililoikumba Pakistan.
Mnamo Desemba 2014, wanamgambo wenye mafungamano na
Taliban waliwaua zaidi ya watu 150, wengi wao wakiwa watoto, katika shambulizi
kwenye shule moja katika mji wa Peshawar kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Ungana nasi katika WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment