Baadhi ya watu huona ugumu kujiwekea akiba kwa sababu
mbalimbali: kipato kisichotosheleza, kuongezeka kwa mahitaji ya nyumbani,
gharama za biashara, madeni mengi au muda mfinyu wa kuangalia mipango ya
uwekezaji iliyopo sokoni.
Lakini kipato chako hata kikiwa kidogo kiasi gani,
hakuna kisingizio cha kuchelewa kuweka akiba. Unaweza kukuta ugumu kidogo
katika jambo hili kwa sababu utahitaji kubadilisha mtindo wa maisha yako, lakini
ina faida nyingi ambazo zinapaswa kukusukuma kulifanya.
Kuna njia kayaya za kujiwekea akiba, lakini kwanza
unahitaji mpango. Hapa tunakuletea dondoo za kutengeneza mpango wa kuweka
akiba:
1. ANZA MARA MOJA
Hakuna muda maalum wa kuanza kuweka akiba. Unapoamua kuweka
akiba, anza mara moja kulingana na mpango wako.
2. TENGA KIWANGO CHA AKIBA
Fanya uamuzi wa kiwango fulani cha mapato yako ya kila
mwezi unachotaka kuweka akiba. Kwa mfano umeamua kuweka asilimia 10. Ili
kufanikisha kutoka kwenye 0 kwenda 10, unaweza kuanza kuweka asilimia 3 katika
mwezi wa kwanza, kisha ongea kiwango hicho mpaka asilimia 6 baada ya miezi 3 na
hatimaye ongeza mpaka asilimia 10 baada ya miezi sita. Kama una umri wa zaidi
ya miaka 50, unaweza kuhitaji kutenga asilimia 20 ya kipato chako na kukiweka katika
akiba yako.
3. JILIPE KWANZA
Unapopokea mshahara wako, punguza asilimia 10 kwanza
kabla ya mambo mengine. Ikiwezekana, weka akiba yako kwenye akaunti maalum ya
benki.
4. ONGEZA ZAIDI AKIBA YAKO
Ainisha gharama zako kulingana na mahitaji yako. Kiasi kinachobaki
kiweke kwenye akaunti ya akiba yako. Unaweza kupunguza mahitaji yako, usisite
kufanya hivyo. Ukipata mgao kwenye biashara yako mwishoni mwa mwaka, unaweza
kuamua kujilipa kwa kuuweka mgao huo kwenye akiba yako.
5. FUATILIA MPANGO WAKO
Fuatilia maendelea ya akiba yako. Unaweza kuamua
kuchukua kiasi fulani cha pesa yako na kukiwekeza kwenye biashara mbalimbali za
uhakika kulingana na malengo yako. Iwapo mpango wako wa kuweka akiba hautaenda
vizuri kwenye miezi ya mwanzo, usikate tamaa. Wakati fulani gharama halisi
zinaweza kuvuka bajeti. Badala ya kukanganyikiwa, chunguza matumizi yako na
uyarekebishe kulingana na mpango wako.
Inaweza kuchukua muda kufanya marekebisho kabla ya
kufikia lengo lako. Kitu muhimu kabisa ni kuanza kutekeleza utaratibu huo wa
kujiwekea leoleo.
Mzizima 24 WhatsApp: +255 626 603 852
0 comments:
Post a Comment