MOGADISHU, SOMALIA – Mlipuko mkubwa wa bomu lililotegwa
kwenye gari na ambao ulilenga kituo cha ukaguzi jirani na Makao ya Rais katika
mji mkuu wa Somalia umewaua watu wasiopungua watano na kuwajeruhi wengine
kadhaa.
Maafisa wa usalama waliokuwa kwenye eneo la tukio
wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kituo hicho cha ukaguzi
kilishambuliwa na bomu lililotengwa kwenye gari ambayo ilikuwa ikiendeshwa na
mshambuliaji wa kujitoa mhanga na kusababisha mlipuko nje ya ukumbi mmoja wa mikutano.
"Kwa uchache watu watano wameuawa wakiwemo maafisa
wa usalama na wengine 10 wamejeruhiwa,” amesema Abdifatah Omar Halane, msemaji serikali
ya Mogadishu.
Afisa wa polisi bwana Mohamed Hussein amesema: "Idadi
ya vifo inaweza kuongezeka. Wakati wa mlipuko kuna watembea kwa miguu waliokuwa
wakipita mahala hapo."
Mtangazaji wa Radio Kulmiye, Farhio Hussein, ameliambia
shirika la habari la Al Jazeera kuwa waathirika ni pamoja na askari wa serikali
waliokuwa kwenye kituo hicho cha ukaguzi katika eneo la katikati ya mji wa Mogadishu.
Eneo la mlipuko lilikuwa karibu na lango la pili la Makazi ya Rais.
"Nilikuwa kwenye kituo cha redio nikasikia mlipuko
mkubwa. Nilipofungua dirisha niliona moshi mkubwa. Nilihesabu miili mitano
ikiwa imelala katika eneo hilo,” alisema Hussein.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo.
Kundi la Al-Shabab lenye uhusiano na Al-Qaeda, ambalo
limekuwa likipambana kuiondosha serikali ya Somalia, limekuwa likilaumiwa kwa mlolongo
wa mashambulizi katika jiji la Mogadishu.
Mwaka 2011 majeshi ya Umoja wa Afrika yalilifurusha
kundi hilo katika mji wa Mogadishu lakini bado linadhibiti maeneo mbalimbali ya
mikoani na kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali, jeshi na ya umma
katika jiji hilo na katika miji mingine.
0 comments:
Post a Comment