Treni imegongana na basi la shule katika kivuko kimoja
kaskazini mwa India leo Alhamisi na kuua watoto 12, polisi ya nchi hiyo
imesema.
Afisa mwandamizi wa polisi O.P. Singh amesema dereva wa
basi hilo naye amepoteza maisha.
Watoto wengine 12 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na
kupelekwa hospitali ya mji wa Kushinagar, kilometa 200 (maili 125) kusini
mashariki mwa Lucknow, mji mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh.
Wanafunzi hao walikuwa wakielekea shule wakati treni
ilipoligonga basi lao.
"Waathrika wengi walifariki dunia hapohapo," afisa
wa polisi katika eneo hilo, Ramkrishna
Tiwari, amesema.
Watoto hao walifariki dunia wote walikuwa na umri chini
ya miaka 10, alisema. Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na baadhi ya
majeruhi kuwa katika hali mbaya.
Polisi imemtupia lawama dereva kwa ajali hiyo. "Ajali
hiyo imetokea kwa sababu ya uzembe wa dereva. Alikuwa ameweka spika masikioni
akisikiliza muziki na hakusimamisha basi kuangalia kama treni ilikuwa inakuja,"
amesema Tiwari.
Mamlaka za serikali katika jimbo hilo zimeagiza
kufanyika uchunguzi huku viongozi wa India wakituma salamu za rambirambi kwa
familia za waathirika hao.
Wazazi na ndugu walioshtushwa na tukio hilo walikimbilia
kwenye eneo la tukio na hospitalini baada ya kusikia taarifa za ajali hiyo.
Matukio ya ajali yamekuwa mengi katika vivuko vya reli
nchini India. Zaidi ya watu milioni 23 hupanda treni za abiria 11,000 nchini
humo kila siku.
Mamia ya vivuko hayana alama, hususan katika maeneo ya
vijijini. Uhaba wa fedha hutatiza uwezo wa huduma za reli kuweka alama au
walinzi katika vivuko hatari kwa wakati.
Madereva wa magari mara nyingi hujaribu kuvuka kwa kasi
katika maeneo ya reli yasiyowekewa alama na hivyo kusababisha ajali.
Hii ni ajali kubwa ya pili kuwahusisha watoto wa shule
katika kipindi cha chini ya wiki mbili.
Mnamo Aprili 9 watoto wasiopungua 24 na watu wazima 3
walipoteza maisha baada ya basi la shule kupata ajali katika barabara ya
mlimani katika jimbo la Himachal Pradesh kaskazini mwa India.
0 comments:
Post a Comment