Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza
kuahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika kesho
Septemba 1.
Viongozi wa chama hicho, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa, wametangaza hatua hiyo kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika leo
jijini Dar es Salaam.
Wamesema wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha
mwezi mmoja ili kuitikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine
waliowaomba kuyapa nafasi mazungumzo.
Viongozi wa chama hicho walikuwa wameitisha maandamano
na mikutano ya kisiasa Septemba Mosi kupinga walichosema kuwa ni ukandamizaji
dhidi ya demokrasia unaofanywa na serikali.
Baada ya mkutano wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho mwishoni mwa mwezi Julai, viongozi walisema:
"Yapo Matukio ambayo yamekua yakifanywa na kukandamiza demokrasia na
misingi ikipuuzwa na kudharauliwa."
"Si nia ya Chadema kugombana na Serikali bali ni
kazi ya Chama Pinzani kuisaidia Serikali iongoze kwa kufuata misingi ya
Katiba," chama hicho kilisema.
Maandamano hayo yalipewa jina Ukuta, ikiwa ni kifupi cha
Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania.
Serikali ilipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa, ya
hadhara na ya ndani. Baadhi ya viongozi wa upinzani wamekamatwa na kuzuiliwa
kwa muda.
0 comments:
Post a Comment