RAIS wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek
Machar wamefikia muafaka wa amani baada ya mgogoro uliodumu kwa miezi mitano.
Muafaka huo unataka kusimamisha mapigano mara moja na
kuunda serikali ya mpito kabla ya kutengenezwa kwa katiba mpya na kufanyika kwa
uchaguzi.
Mgogoro huo umegharimu maisha ya maelfu ya watu na zaidi
ya milioni moja kukosa makazi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry,
ambaye alifanya juhudi kubwa kuzileta pamoja pande mbili za mgogoro amesema
kuwa muafaka huo ni ishara nzuri kwa mustakblai wa Sudan Kusini.
Kerry amesema kuwa safari ngumu na ndefu katika taifa
hilo inaanza sasa na inapaswa kuendelea, akiongeza kuwa watu wa Sudan Kusini
wameteseka kwa muda mrefu.
Umoja wa Mataifa umezituhumu pande mbili zinazohusika na
mgogoro huo kwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya
halaiki na magenge ya ubakaji.
Mahasimu hao wamesaini makubaliano hayo mjini Addis
Ababa, Ethiopia jana, baada ya mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana kuanza.
Taarifa zinasema kuwa muafaka huo unatoa wito wa
kusimamisha mapigano ndani ya saa 24 baada ya kusainiwa na kisha makubaliano ya
kudumu yatasainiwa.
Kiir na Machar walitarajiwa kutoa maagizo mara moja kwa
vikosi vyao kuacha mapigano na kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu.
Haijawa wazi nani atakayeunda serikali hiyo ya mpito
iliyoelezwa katika vifungu vya muafaka huo.
0 comments:
Post a Comment