KATIBU
wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, ataendelea kukaa
mahabusu hadi pale jalada la kesi yake litakaporejeshwa kutoka Mahakama Kuu.
Akiahirisha
kesi hiyo jana hadi Aprili 16, Hakimu mkazi mkoani Morogoro, Marry Moyo,
aliitaka Idara ya Upelelezi kufuatilia jalada la mtuhumiwa Mahakama Kuu ili
kesi ianze kusikilizwa.
Sheikh
Ponda anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Batheromeo Tharimo alifikishwa
mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali licha ya kutokuwepo umati mkubwa wa
wafuasi wake.
Mara
baada ya kufikishwa, wakili wake Tharimo alidai kuwa amewasiliana na wakili
mwenzake Juma Nassoro ambaye alimweleza kuwa kuna ombi waliliwasilisha Mahakama
Kuu la kutaka shauri hilo kutoendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa wa
Morogoro.
Katika
ufafanuzi wake juu ya madai hayo, Tharimo alisema kuwa ombi hilo linatokana na
rufaa namba 98 ya mwaka 2013 waliyoikata mbele ya Mahakama Kuu kuhusu Mahakama
ya Kisutu kwa shitaka la kwanza la kutotii amri halali linalomkabili Ponda
mahakamani hapo.
Wakili
huyo ambaye alidai kuwa uendeshaji wa kesi hiyo hautaendelea hadi uamuzi wa
rufaa waliyoikata Mahakama Kuu utakapotolewa, aliiomba mahakama kupanga tarehe
ya kutaja kesi hiyo.
Hata
hivyo, uliibuka ubishani wa kisheria baina ya wakili Tharimo na wakili wa
serikali, Sunday Hiela, aliyedai ana kumbukumbu za kuonyesha mshtakiwa alimkana
wakili Tharimo.
Katika
maelezo yake Hiela aliongeza kuwa mahakama inashindwa kujua kama anamwakilisha
Sheikh Ponda au anatoa maelezo ya wakili Juma Nassoro ambaye hakuwepo
mahakamani hapo.
Wakili
huyo wa serikali aliendelea kumwekea pingamizi akidai kuwa hakuna nakala yoyote
ya ombi ambalo wakili Tharimo alidai kuwa waliliwasilisha Mahakama Kuu na
kwamba dhamira ya upande wa utetezi ni kuchelewesha kesi hiyo ambayo ipo
mahakamani hapo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Kufuatia
kuwepo kwa mapingamizi katika kesi hiyo, hakimu Moyo alilazimika kuingilia kati
akisema hadi sasa mahakama bado haijapokea jalada hilo kutoka Mahakama Kuu ili
ipate muongozo wa kuendelea na kesi hiyo.
Baadaye
aliihairisha kesi hiyo hadi Aprili 16 itakapotajwa tena, ingawa wakili Tharimo
aliomba kesi hiyo itajwe Aprili 14 kwa madai kuwa hatakuwepo kutokana na kuwa
na kesi nyingine.
Sheikh
Ponda alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 10, 2013
akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kutotii amri halali iliyotolewa
Mahakama ya Kisutu, kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini na
kushawishi watu kutenda kosa.
0 comments:
Post a Comment