Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Madawa (TFDA), Hiiti Sillo (kushoto),akiwaonyesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, maziwa ya watoto yaliyokamatwa kwenye maduka makubwa nchini . |
Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imekamata na
kuyaharibu makopo 591 ya maziwa ya watoto katika maduka 36 yenye thamani ya Sh.
17,625,000 ambayo hayajasajiliwa na kutokuwa na maelezo ya lugha ya Kiswahili.
Hatua hiyo imetokana na kuvunjwa kwa sheria na kanuni ya
Maziwa ya Watoto ya mwaka 2013 ya TFDA ambayo inasema lugha isiyo ya Kiswahili
na michoro ya picha inayomshawishi mnunuzi hairuhusiwi katika bidhaa hiyo.
Maziwa hayo ambayo yamekutwa yakiuzwa katika maduka na
mengine katika supermarket mbili za Kichina na kuwa na maelezo ya lugha ya
Kichina ni aina ya SMA ( 1, 2,3), S-26 Gold, Promil Gold, Progress Gold, Cow
& Gate, Infacare Soya, Isomil 2, Nutrikids, Nursory na Aptimil 1.
Mkurugenzi Mkuu TFDA, Hiiti Sillo, alisema hatua hiyo
imechukuliwa baada ya mamlaka hiyo kufanya ukaguzi katika maduka, bakery na
supermarket uliofanyika kati ya Machi 10 na 21, mwaka huu katika mkoa wa Dar es
Salaam.
Alisema kuwa maziwa ya watoto yaliyosajiliwa na TFDA
kisheria yanatakiwa kuwa na maelezo yenye lugha mbili ya Kiswahili na
Kiingereza ili kumwezesha mtumiaji wa bidhaa hiyo kutoa kipimo cha matumizi
sahihi kwa mujibu wa mtengenezaji.
Aidha, alisema ukaguzi huo uliofanyika katika
supermarket 107 kwa kushirikiana na wakaguzi wa Manispaa za Ilala, Kinondoni na
Temeke, umetokana na kukithiri kufunguliwa maduka hayo ikiwamo kuingizwa kwa
bidhaa ambazo hazijasajiliwa, hatua ambayo ni kinyume cha sheria.
Mbali na kuharibiwa kwa maziwa hayo, pia makopo na
paketi 6,090 za chumvi zenye ujazo tofauti zenye thamani ya Sh. 5,131,000
zilikamatwa katika maduka 39 kutokana na kutosajiliwa na TFDA.
Alizitaja aina ya chumvi hizo ambazo ni Ken Salt,
American Garden Salt, Lo Salt, Chilly Willy Salt, Today’s Essential, Best Salt,
Nezo Salt, DP, Costa Salt na kusema zinauzwa katika maduka hayo kwa kukiuka
kanuni ya uwekaji wa madini joto ya mwaka 2010.
Pia, alisema bakery nne ndani ya supermarket zilikutwa
hazina vibali pamoja na maduka 12 ambayo yalikutwa yakiuza vinywaji baridi vya
kuongeza nguvu ambavyo havijasajiliwa na mamlaka hiyo. Vinywaji hivyo ni B52,
Red Bull (silver, red, blue), Boost, Krazy, Monster, Rockstar, Climax na Atlas.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment