RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete,
amechaguliwa kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo barani
Afrika kwa mwaka 2013.
Heshima hiyo kwa Rais Kikwete imetolewa na jarida
maarufu la kimataifa la ‘African Leadership Magazine Group’ na tuzo ya heshima
hiyo ilitarajiwa kutolewa jana jioni Aprili 9, 2014, katika sherehe
zilizopangwa kufanyika katika Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C ikiwa
ni pamoja na chakula cha jioni.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, ilisema kuwa tuzo hiyo itapokewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye tayari
amewasili mjini Washington kwa sherehe hizo kubwa.
Tuzo hiyo ya heshima kubwa hutolewa kwa viongozi wa
Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa
watu wao na imetolewa kwa Rais Kikwete kutokana na mwelekeo wake usiokuwa wa
kawaida na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora.
Jarida hilo linasema kuwa ukweli wa hali hiyo bora ya
utawala bora chini ya uongozi wa Rais
Kikwete umeendelea kumiminiwa sifa kimataifa na leo umeifanya Tanzania kuwa
nchi ya kuigwa mfano kama kituo cha uhakika cha uwezeshaji kutokana na mageuzi
makubwa yaliyofanywa katika sera na mifumo ya uchumi.
Jarida hilo linasema kuwa Rais Kikwete alikuwa chaguo
kubwa na la kwanza la wasomaji wa jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia
mbali mbali za mawasiliano za jarida hilo.
Linasema jarida hilo: “Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu
ya kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na
maendeleo, matokeo ya majibu ya swali hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote
kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila
mahali – ameweza kusimamia uchumi ambao umekua kwa wastani wa asilimia saba kwa
miaka yote ya uongozi wake.”
Jarida hilo litaweza kutangaza mafanikio ya Tanzania
chini ya uongozi wa Rais Kikwete kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na
Jumuiya ya Kimataifa ya Kibiashara, wanadiplomasia na taasisi nyingine zenye
ushawishi mkubwa katika medani za kimataifa na zenye makao yake katika Jiji la
Washington na maeneo ya jirani.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment