Rais wa zamani wa Ufaransa na kiongozi wa chama cha Les
Republicains, Nicolas Sarkozy
PARIS
RAIS wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, anashikiliwa
na jeshi la polisi la nchi hiyo kwa tuhuma za matumizi ya fedha chafu wakati wa
kampeni yake ya kugombea urais wa nchi hiyo mwaka 2007.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, hivi karibuni Sarkozy
alihojiwa na polisi mjini Nanterre ikiwa ni sehemu ya uchunguzi dhidi ya tuhuma
za kupewa fedha na utawala wa zamani wa Libya kwa ajili ya kampeni zake za
urais za mwaka 2007, gazeti la Le Monde la nchini humo limeripoti.
Hii ni mara ya kwanza kwa Sarkozy kuhojiwa katika
uchunguzi huo ambao ulianza miaka mitano iliyopita. Anaweza kuendelea
kushikiliwa na polisi kwa muda usiozidi saa 48 na kisha anaweza kupelekwa
mahakamani kwa ajili ya mashitaka rasmi.
Majaji Serge Tournaire na Aude Buresi wamekuwa
wakishughulikia kadhia hiyo tangu Aprili 2013 ili kubaini iwapo kampeni hizo za
Sarkozy zilihusisha fedha haramu kutoka Libya.
Mnamo Juni 2016, majaji wa Ufaransa walitoa uamuzi kuwa
nyaraka zinazodai kuwa Sarkozy alipewa Yuro milioni 50 na kiongozi wa zamani wa
Libya, Kanali Muammar Gaddafi kama msaada kwa kampeni zake za uchaguzi, ni
nyaraka sahihi.
Nyaraka hizo zilizofichuliwa kwa mara ya kwanza na
mitandao ya habari za kiuchunguzi nchini humo mwaka 2012, zinadaiwa kuonyesha
kuwa Sarkozy alifanya makubaliano na Gaddafi kwa ajili ya kufadhili kampeni
zake za urais katika uchaguzi huo ambao alimshinda Segolene Royal kutoka chama
cha kisoshalisti.
Mwaka 2016 gazeti la kila siku la Le Monde katika
machapisho matatu mtawalia liliripoti juu ya "uwepo wa mtandao mkubwa wa
kiuhalifu uliowahusisha maafisa waandamizi wenye ukaribu na Sarkozy.
" Mtandao huu, ambao ulikuwa na kazi ya kumlinda rais
huyo wa zamani, unaundwa na maafisa wa polisi na mahakimu ambao waliendelea
kuwa watiifu kwake, lakini pia uliwahusisha wafanyabiashara, watu wa kati,
wanadiplomasia na hata waandishi wa habari," gazeti hilo liliripoti.
Mtandao huo ulidaiwa kuundwa baada ya Sarkozy kuwasili
wizara ya mambo ya ndani mwaka 2002, ambapo uliimarishwa zaidi baada ya kuingia
Ikulu ya Elysee mwaka 2007.
Aidha, mnamo Septemba 2016, waendesha mashitaka walishauri
kuwa Sarkozy na wenzake 13 wafikishwe mahakamani kujibu mashitaka ya kutumia
mamilioni ya fedha chafu kufadhili kampeni zake za urais za mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment