KAMPENI ZA UCHAGUZI ZAANZA GUINEA CONAKRY

 Kampeni za uchaguzi zaanza Guinea Conakry





Kampeni za uchaguzi wa bunge zimeanza nchini Guinea Conakry kwa lengo la kuwania viti katika uchaguzi ambao umepangwa kufanyika Juni 30. Wakati huohuo vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya maandamano katika mji mkuu Conakry kwa lengo la kuishinikiza serikali iakhirishe tarehe ya kufanyika uchaguzi huo.

 Katika hali ambayo wapinzani wanasema kuwa watu 15 wameuwa na askari usalama katika maandamano hayo lakini serikali kwa upande wake inasema kuwa ni mtu mmoja tu ndiye aliyepoteza maisha katika mandamano hayo. Wapinzani wamekataa kuwasilisha majina ya wagombea wao katika uchaguzi huo na kuitaka serikali iuakhirishe.

Tokea kutangazwa rasmi tarehe ya kufanyika uchaguzi huo wa bunge katikati ya mwezi Aprili uliopita, mji mkuu wa Guinea Konakry umekuwa ukishihudia makabiliano makali kati ya serikali na wapinzani. Cellou Dalein Diallo kiongozi wa chama cha upinzani cha Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG) ameandamana na mwanasiasa mpinzani mwenzake Lansana Kouyate wa chama cha Party for Hope and National Development, PEDN na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo katika safari yao huko Paris mjini Ufaransa kwa lengo la kuishawishi jamii ya kimataifa izingatie zaidi matukio ya kisiasa ya nchi yao.

Vyama vya upinzani vinamtuhumu Rais Alpha Konde kuwa anafanya njama ya kuiba kura katika uchaguzi ujao. Vinaitaka serikali ijadiliane navyo kuhusiana na udharura wa kuakhirishwa uchaguzi huo hadi mwezi Oktoba au Novemba ili kuandaliwa na kudhaminiwa zaidi mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Wapinzani pia wanapinga vikali kupewa kandarasi ya kuandaa orodha ya wapiga kura na kusimamia shughuli ya kuhesabu kura iliyopewa shirika la Waymark la nchini Afrika Kusini kwa madai kwamba linashirikiana kwa karibu na serikali ili kuiba kura kwa maslahi ya chama tawala.

Licha ya kuwa Tume ya Uchaguzi ya Guinea Conakry imetangaza kuwa iko tayari kuandaa na kusimamia uchaguzi huru na wa haki nchini kufikia tarehe 30 Juni, lakini wataalamu wa mambo wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na suala hilo kwa kuizngatia mivutano na ghasia zinazoendelea nchini humo katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi.

Umoja wa Nchi za Afrika AU na Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS zimeelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusiana na matukio hayo na kuzitaka pande zinazozozana nchini humo kutatua hitilafu zao kwa njia ya mazungumzo. Uchaguzi huo wa bunge ndio hatua ya mwisho ya kukabidhiwa madaraka kwa amani kwa serikali ya kiraia tokea kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi nchini humo mwaka 2008. Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyofanyika kuafuatia kifo cha Lansana Conte yameisababishia nchi hiyo mgogoro mkubwa wa kisiasa.



CHANZO: IRIB
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment