Kwa uchache wakimbizi watano wameuawa na wengine 20
kujeruhiwa kwenye kambi moja nchini Rwanda baada ya maandamano ya kupinga hatua
ya upunguzaji wa chakula kutawaliwa na ghasia, jeshi la polisi nchini humo
limesema. Polisi saba pia walijeruhiwa.
Wakimbizi wapatao 3,000 waliweka kambi nje ya ofisi za
Umoja wa Mataifa kwenye kambi hiyo tangu Jumanne. Siku ya Alhamisi polisi
walijaribu kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, msemaji wa polisi Theos
Badege ameiambia redio ya serikali.
“Tulitumia nguvu jana mchana baada ya kutoa onyo kwamba
vikosi vya usalama vitatumika,” alisema.
“Walianza kurusha mawe na vyuma, na hapo wakimbizi 20 na
maafisa saba wa polisi wakajeruhiwa. Wakimbizi watano walifariki dunia.”
Wakimbizi kumi na tano walikamatwa, jeshi la polisi limesema
kupitia mtandao wa Twitter.
Wakimbizi hao kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo waliondoka kambini katika eneo la Kiziba na kutembea kwa
miguu umbali wa kilometa 15 (maili 10) mpaka Karongi, magharibi mwa Rwanda, kupinga
hatua ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kukata
asilimia 25 ya mgao wa chakula mwezi uliopita. Kambi hiyo inawahifadhi
wakimbizi 17,000 kutoka Kongo.
Rwanda imewahifadhi wakimbizi wapatao 174,000, wakiwemo
wakimbizi 57,000 kutoka nchi jirani ya Burundi ambao walikimbia ghasia nchini
mwao mwaka 2015. Wengine waliobaki waliikimbia Kongo kwa sababu za ukosefu wa
uthabiti nchini mwao zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Mnamo mwezi Januari, UNHCR ilisema kuwa ingepunguza mgao
wa chakula kutokana na uhaba wa ufadhili wa huduma zake.
Mapema Alhamisi shirika hilo lilisema ilipokea asilimia
2 tu ya ufadhili kwa mwaka 2018 kwa ajili ya huduma zake nchini Rwanda ambao ni
dola milioni 98.8, huku Shirika la Chakula Duniani likionya kuwa litapunguza
zaidi chakula iwapo mahitaji yake ya kila mwezi ya dola milioni $2.5 hayatotekelezwa.
0 comments:
Post a Comment