Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai,
amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 65 kutokana na saratani, maafisa wa
chama chake wamesema.
Makamu wa rais wa chama cha Movement for Democratic
Change (MDC), Elias Mudzuri, alitoa taarifa ya kifo cha Tsvangirai kupitia mtandao
wa Twitter mapema Jumatano usiku.
"Ninasikitika kutangaza kwamba tumempoteza kinara
wetu na mpiganiaji wa demokrasia," aliandika Mudzuri.
Tsvangirai alikuwa akienda mara kwa mara katika
hospitali nchini Afrika Kusini baada ya kundulika kuwa na maradhi ya saratani
ya matumbo mwaka 2016.
Aliwahi kuwa waziri mkuu chini Rais wa zamani wa nchi hiyo
Robert Mugabe katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa mwaka 2009 mpaka 2013.
Naye msemaji wa chama chake, Obert Gutu, alithibitisha
taarifa za kifo cha Tsvangirai kupitia mtandao wa Twitter, akimuelezea kama "kinara
wa kisiasa, mtu mnyenyekevu na mpambanaji asiyechoka aliyepigania taifa lenye
amani, uthabiti, demokrasia na maendeleo nchini Zimbambwe".
Wiki iliyopita, Tsvangirai aliingia kwenye mtandao wa Twitter
na kuelezea kuwa maradhi yake yalikuwa katika hatua za mwisho.
"Nina saratani na sijisikii vizuri sana, lakini
niko thabiti na maradhi yanadhibitiwa… ninapona,” aliandika mapema Februari 6.
Wananchi katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare,
wameshitushwa na taarifa za kifo chake, huku wakisema kuwa watamkumbuka sana.
MORGAN
TSVANGIRAI NI NANI?
Alikuwa mzungumzaji mahiri. Alizaliwa mwaka 1952 katika
eneo la Buhera, kusini mashariki mwa Zimbabwe. Baba yake alikuwa fundi ujenzi.
Zimbabwe ilipopata uhuru wake kutoka kwa Muingereza
mwaka 1980, Tsvangirai alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi
Migodini, akipanda ngazi mbalimbali mpaka kuwa katibu mkuu wa Baraza la Vyama
vya Wafanyabiashara nchini humo (ZCTU) mwaka 1988, nafasi ambayo aliachana nayo
baada ya kuunda chama chake cha kisiasa cha Movement for Democratic Change
(MDC) mwaka 1999.
Katika uchaguzi wa mwaka 2008 alikuwa mshindani mkuu wa Mugabe
na chama chake cha ZANU-PF. Alifanikiwa kupata asilimia 47 ya kura dhidi ya asilimia
43 za Mugabe, lakini kura hizo hazikumuwezesha kutawazwa kuwa mshindi wa moja
kwa moja, na hivyo uchaguzi wa marudio ulitangazwa.
Tsvangirai aligomea uchaguzi wa marudio, akielezea
vitisho na unyanyasaji dhidi ya wafuasi wake, na hivyo kumfanya Mugabe kuwa
mshindi.
Viongozi wa kanda na wale wa jumuiya ya kimataifa
waliingilia kati, na baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo Tsvangirai aliapishwa
kama waziri mkuu mwaka 2009. Ilikuwa serikali ya muda ya kugawana madaraka,
lakini Mugabe aliendelea kuwa rais.
Katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2013, chama cha
Tsvangirai kilishindwa vibaya. Wakosoaji wake walisema kuwa alikuwa amesahau
shida za masikini na kutamalakiwa na ulevi wa mali na madaraka.
Kifo cha Tsvangirai kimetokea ikiwa ni miezi michache
kabala ya Wazimbabwe kuelekea kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais mpya
kufuatia kujiuzulu kwa Mugabe, ambaye amerithiwa na Emmerson Mnangagwa.
Wachambuzi wa siasa za Zimbabwe wanasema kuwa kifo cha Tsvangirai
ni pigo kubwa kwa upinzani nchini humo.
Wanasema kuwa kumpata mtu mpya na kujaribu kujenga jina
lake nchini ndani ya kipindi cha miezi minne ni kazi ngumu sana.
0 comments:
Post a Comment