Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte |
Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amekosolewa vikali
na mashirika ya haki za binadamu baada ya kusema kuwa waasi wa kike wa kundi la
kikomunisti nchini humo wanatakiwa kupigwa risasi katika sehemu zao za siri
kama adhabu yao kwa kufanya uasi dhidi ya serikali.
Tangazo la Duterte ni sehemu ya mfululizo wa kauli zenye
utata alizozitoa kuhusu wanawake, shirika la haki za binadamu la Human Rights
Watch limesema katika tamko lake.
"Ni kauli inayowahamasisha askari wa serikali
kufanya dhulma za kijinsia katika uwanja wa mapambano, jambo ambalo ni ukiukaji
wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu," amesema mwakilishi wa Human
Rights Watch nchini humo bwana Carlos Conde.
Kwa mujibu wa hotuba iliyotolewa Februari 7, bwana Duterte
alisema kuwa askari wa serikali wanatakiwa kuwapiga risasi waasi wa kike sehemu
zao za siri.
"Tutawapiga risasi kwenye sehemu zenu za siri, ili
kwamba ukikosa sehemu za siri, msiwe na faida yoyote," alisema Duterte katika
lugha ya kikabila ya Visayan, ambayo huzungumzwa katika eneo la kati na kusini
mwa Ufilipino.
Aidha, rais huyo aliwalaumu vikali wanawake hao waasi
kwa kuwatekeleza watoto na familia zao na kwenda kujiunga na kikundi hicho cha
waasi wa kikomunisti.
Emmi de Jesus, mbunge kutoka chama cha Wanawake cha Gabriela
Women's Party, alilaani vikali kauli tata ya Duterte na kusema kuwa itachangia
kueneza utamaduni wa uvunjaji wa sheria nchini humo.
MSEMAJI: DUTERTE ANAPENDA SANA UTANI
Duterte amekosolewa mara kadhaa kwa kauli zake zenye
utata dhidi ya wanawake.
Mwezi Januari, wakati wa ziara yake nchini India,
aliwaambia wafanyabiashara wakubwa wa India na Ufilipino mjini New Delhi kuwa
angependa kuwavutiwa wawekezaji kuwekeza katika nchi yake kwa kuwapa ofa ya wanawake
bikra 42.
Mnamo Julai 2017, alifanya utani wa vitendo vya ubakaji
kuhusu Miss Universe.
Miezi miwili kabla, Duterte aliwaambia askari waliokuwa
wakipigana na wapiganaji wa Kiislamu katika eneo la Marawi kuwa wakitaka
wanaweza kubaka wanawake watatu na hawatoadhibiwa.
"Nitawafunga jela mimi mwenyewe," alisema,
akitoa tahadhari kwa askari wanaokiuka sheria. Kisha akasema: “Lakini ukibaka
wanawake watatu, nitakubali, sitakuwa na shida nalo hilo.”
Wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2016, wakosoaji
wake walikasirishwa sana alipoelezea tukio la ghasia za gereza moja lililotokea
mwaka 1989 ambapo Mmisionari mmoja wa Kiaustralia aliuawa, na wafungwa
walipanga msitari kwa ajili ya kumbaka.
Duterte alisema kuwa mwanamama huyo alikuwa “mrembo” na
yeye kaka meya wa mji wa Davao lilikotokea tukio hilo, alitamani kuwa wa kwanza
kupanga foleni kumbaka mwanamke huyo. Baadaye aliomba radhi na kusema kuwa
hakukusudia kuvunja heshima ya wanawake au waathirika wa ubakaji.
Mapema Jumatano, msemaji wa Duterte, Harry Roque, alitetea
kauli tata za rais huyo akisema kuwa wakosoaji wake wanapaswa kuwa waelewa.
"Unajua, wakati mwingine, watetezi hawa wa mambo ya
wanawake wanakuwa na mhemko sana”, alisema Roque.
"Ninamaanisha kuwa huo ni mzaha tu. Msikuze mambo. Furahini
basi,” alisema msemaji huyo wa Duterte.
Utawa wa Duterte umekuwa ukifanya mazungumzo ya mara kwa
mara ya kusaka amani na waasi hao wa kikomunisti tangu alipoingia madarakani
katikati mwa mwaka 2016.
Lakini kufuatia kuibuka kwa mapambano mapya kati ya
vikosi vya serikali na waasi hao mwaka 2017, Duterte alisaini tangazo
lililowaorodhesha waasi hao kama kundi la kigaidi, na hivyo kukatisha mchakato
wa kusaka amani.
Pia aliagiza kutiwa nguvuni kwa viongozi kadhaa wa
kikomunisti.
Chama hicho cha Kikomunisti kilianza uasi nchini humo
kwa 1968 ambapo mpaka sasa zaidi ya watu 30,000 wamepoteza maisha.
|
0 comments:
Post a Comment