Maafisa wamezifunga barabara zinazoelekea katika Chuo cha kijeshi cha Jemedari Faheem baada ya shambulizi lililotokea leo mjini Kabul. |
Chuo kimoja cha jeshi katika mji mkuu wa Afghanistan,
Kabul, kimeshambuliwa na kusababisha askari wawili kupoteza maisha, siku chache
baada ya zaidi ya watu 100 kuuawa katika mlipuko jirani na jengo la wizara ya
mambo ya ndani.
Msemaji wa ikulu ya nchi hiyo amesema kuwa washambuliaji
hao hawakuweza kuingia ndani ya Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Taifa cha Jemedari Fahim
– ambalo ni shambulio kubwa la tatu katika mji huo ndani ya wiki mbili.
Shambulizi hilo limedaiwa kufanywa na kundi la
wapiganaji wa Dola la Kiislamu katika Iraq na Sham (ISIL) kupitia tovuti ya
kundi hilo ya Amaq.
Aidha, mbali na askari hao wawili, kwa uchache askari 10
wamejeruhiwa, huku washambuliaji wanne wakiuawa na mmoja kukamatwa.
Mashambulizi yanaendelea katika kikosi cha polisi jirani
na chuo hicho, maafisa wamesema.
Shambulizi la leo limetokea wakati wakazi wa mji huo
wakiwa na maumivu kutokana na shambulizi la kujitoa mhanga lililotokea siku ya
Jumamosi katika eneo la katikati ya mji, ambalo liliua zaidi ya watu 100 na
wengine 91 kujeruhiwa.
Mji wa Kabul tayari ulikuwa kwenye tahadhari kubwa, huku
ulinzi ukiimarishwa hasa jirani na eneo la mlipuko huo – eneo la karibu na
jengo la wizara ya mambo ya ndani, hospitali ya Jamhuriat, ofisi za serikali,
maeneo ya biashara na shule.
Kundi la Taliban lilidai kuhusika na shambulizi la
Jumamosi, likisema kuwa liliwalenga maafisa wa serikali.
Abdullah Fahimi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Abu Rayhan mjini
Kabul, aliliambia shirika la habari la Al Jazeera kuwa mji huo umeshuhudia
ongezeko kubwa la mashambulizi yanayofanywa na makundi ya waasi katika misimu
miwili ya majira ya baridi iliyopita.
"Haya yanatokea kutokana na mkakati mkali
uliofanywa na serikali ya Afghanistan na serikali ya Marekani, ambazo
ziliwawekea vikwazo wanachama sita wa kundi la Taliban Mtandao wa Haqqani,"
Fahimi amesema.
Taarifa zaidi itawajia...
CHANZO: Aljazeera
0 comments:
Post a Comment