Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte akionesha picha ya mfanyakazi wa Kifilipino aliyekuwa akifanya kazi nchini Kuwaita, ambaye anasema kuwa alichomwa kama nguruwe, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Davao, katika kisiwa cha kusini mwa nchi hiyo cha Mindanao Februari 9, 2018. |
Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amesema kuwa anataka
wafanyakazi wa Kifilipino kuondoka nchini Kuwait ndani ya saa 72 baada ya
mtumishi wa kazi za ndani raia wa Ufilipino kukutwa amekufa na kuwekwa ndani ya
jokofu katika nyumba moja isiyokaliwa na watu katika taifa hilo la Ghuba.
Duterte amesema kuwa ameiagiza Wizara ya Kazi kufanya
uratibu na mashirika ya ndege ya Ufilipino kuwapatia tiketi za bure wafanyakazi
wa Kifilipino walioko nchini Kuwait ambao wanataka kurejea nyumbani.
"Ninataka waondoke (Kuwait), wale wanaotaka
kuondoka, ndani ya saa 72," aliwaambia waandishi wa habari. "Tutahesabu
uhai wetu kwa saa kwa sababu ni dhahiri kuwa kila saa moja Wafilipino
wanafanyiwa mateso, dhulma na ukatili."
Mnamo mwezi Januari, Ufilipino ilisitisha zoezi la
kupeleka wafanyakazi nchini Kuwait baada ya kutokea kwa vifo vyenye utata dhidi
ya Wafilipino katika miezi ya hivi karibuni.
Duterte alisema kuwa marufuku hiyo itaendelea mpaka pale
serikali itakapokuwa na uhakika kwamba kuna usalama kwa wafanyakazi nchini
Kuwaita ambako Wafilipino 103 walifariki dunia mwaka 2017, kutoka watu 82
waliopoteza maisha mwaka 2016.
"Niko tayari kuchukua hatua kali zitakazosaidia
kulinda uhai na maisha ya Wafilipino," alisema. "Hatuna nia ya
kuikosea serikali yoyote au mtu yeyote. Lakini kama zuio linahitajika, basi
liendelee tu."
"Zuio linaendelea sasa na sijui litaendelea mpaka
lini," aliongeza.
Mnamo siku ya Jumanne, mwili wa mfanyakazi wa ndani
mwenye umri wa miaka 29 aitwaye Joanna Daniela Demafelis ulikutwa ndani ya
jokofu nchini Kuwait, ambako Wafilipino wapatao 250,000 wanafanya kazi na
kuishi. Kwa mujibu wa Durtete, mwili wa mwanamke huo ulikuwa na alama za mateso
na ilionekana kuwa amenyongwa.
0 comments:
Post a Comment