Nyota wa Klabu ya soka ya Real Madrid ya nchini
Hispania, Cristiano Ronaldo anatarajiwa kufika mahakamani baada ya waendesha
mashitaka nchini humu kumtuhumu kukwepa kodi ya kiasi cha zaidi ya Yuro milioni
14, na kumfanya kuwa katika orodha ya wachezaji waliokumbana na mkono wa
mamlaka za nchi hiyo.
Msemaji wa timu ya wanasheria wa Ronaldo mwenye umri wa
miaka 32, amesisitiza kuwa nyota huyo raia wa Ureno atafika mahakamani
mwenyewe, huku akikataa kueleza kwa undani zaidi.
Nyota huyo ambaye jarida la Forbes limemtaja kama
mwanasoka anayeingiza pesa nyingi duniani, sio wa kwanza kutuhumiwa kukwepa
kodi nchini Hispania, kwani miongoni mwao wapo wanasoka kadhaa akiwemo mpinzani
wake mkubwa, nyota wa Barcelona, Lionel Messi.
Mwaka jana Messi na baba yake walihukumiwa kifungo cha
miezi 21 kwa kosa la kukwepa kodi yenye thamani ya Yuro milioni 4.16. Hata
hivyo, mwezi Julai mwaka huu mahakama iliwabadilishia adhabu kwa kutakiwa
kulipa ziada ya pesa.
Waendesha mashitaka wanamtuhumu Ronaldo kukwepa kodi ya
kiasi cha Yuro milioni 14.17 (sawa na Dola milioni 17.3) na kutumia kampuni
iliyoanzisha mwaka 2010 kuficha mapato aliyoyapata nchini humo kupitia haki za
matangazo.
Mamlaka nchini humo zinaona kuwa alichofanya Ronaldo ni “uvunjifu
wa makusudi wa wajibu wa ulipaji kodi nchini Hispania” kwa kupitia makampuni
yenye makao katika Visiwa vya Virgin nchini Uingereza na mengine huko Ireland
ambayo ni maarufu kwa kupuuzia suala la kodi.
RONALDO
HANA WASIWASI
Aidha, mamlaka nchini humo zinasema kuwa Ronaldo aliweka
wazi mapato yake nchini humo ya kiasi cha Dola milioni 11.5 pekee kati ya mwaka
2011 na 2014, ilhali kiasi halisi cha mapato yake katika kipindi hicho kilivuka
Yuro milioni 43.
Vilevile, mamlaka zinamtuhumu kwamba alikataa kwa
makusudi kuorodhesha mapato ya kiasi cha Yuro milioni 28.4 yenye mafungamano na
haki za matangazo kati ya mwaka 2015 na 2020 kwenye kampuni moja ya Kihispania.
Hata hivyo,
Ronaldo anasisitiza tangu mwanzo kuwa hana hatia, na kwamba aliweka wazi mapato
yake yote na kwa njia rasmi.
Tangu alipoelekezewa tuhuma hizo mwezi Juni mwaka jana,
Ronaldo aliamua kukaa kimya ambapo muda mfupi kabla ya timu yake ya taifa
kushiki michuano ya kombe la mabara nchini Urusi alisema tu kwamba hana
wasiwasi kuhusu suala hilo, ambapo baada ya siku mbili akasema kuwa kukaa kimya
“ni jibu zuri zaidi” dhidi ya tuhuma hizo.
Licha ya upande wa wanasheria kukaa kimya, suala hilo
lilichukua nafasi kubwa katika ulimwengu wa soka, hususan baada ya kufuatiwa na
mfululizo wa ripoto mbalimbali za vyombo vya habari kuhusu nia ya mchezaji huyo
kutaka kuondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo mwaka 2009 akitokea
Manchester United.
Ripoti hizo ziliashiria kuwepo kwa uhusiano kati ya
tuhuma hizo na nia yake ya kuhamia klabu tofauti katika nchi nyingine.
Hata hivyo, baadaye Ronaldo aliweka wazi na kusisitiza
juu ya nia yake ya kubaki katika klabu hiyo ambayo katika msimu uliopita aliiongoza
kutwaa ubingwa wa nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 na kuchukua
kombe la Klabu Bingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo.
Aidha, kocha wa mabingwa hao, Mfaransa Zinadine Zidane
alisisitiza kuwa mchezaji wake huyo angebaki.
Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa masuala ya kodi ya
mapato nchini Hispania, iwapo Ronaldo atapatikana na hatia anaweza kutozwa
faini ya kiasi cha Yuro milioni 28 na anaweza kupewa adhabu ya kifungo cha
miaka mitatu na nusu.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, tangu Ronaldo alipoongeza
mkataba wake na Real Madrid mwezi Novemba 2016 mpaka mwaka 2021, amekuwa
mchezaji mwenye kuongiza mapato makubwa zaidi duniani, na katika msimu wa 2016 –
2017 alipata kiasi kipatacho Dola milioni 93.
0 comments:
Post a Comment