Polisi nchini India imesema kuwa mtu mmoja anashikiliwa
baada ya kundi la watu kumuua kijana wa Kiislamu baada ya kumshuku kuwa amebeba
nyama ya ng’ombe, jambo ambalo ni kosa katika maeneo mengi ya nchi ya India
yenye waumini wengi wa dini ya Kihindu.
Wahindu huwaheshimu na kuwatukuza ng’ombe, na kuchinja
au kula nyama ya ng’ombe ni jambo ambalo limepigwa marufuku katika majimbo
mengi nchini humo, huku baadhi ya majimbo hayo yakiweka adhabu ya kifungo cha
maisha kwa mwenye kukiuka marufuku hiyo.
Junaid Khan mwenye umri wa miaka 15, siku ya Ijumaa
alikuwa akisafiri kutoka New Delhi pamoja na ndugu zake watatu ndipo mapigano
yalipoibuka ndani ya gari.
Wanaume kati ya 15 na 20 walichomoa visu na
kuwashambulia jamaa hao huku wakitoa kauli dhidi ya Waislamu na kusisitiza kuwa
mfuko mmoja waliokuwa wamebeba ulikuwa na nyama ya ng’ombe.
Wakati Khan aliuawa, ndugu yake Shakir alipata majeraha
kooni, kifuani na mikononi, polisi wamesema.
Ndugu yake mwingine, Hassem, aliwaambia wanahabari kuwa
kundi hilo lilipuuza ombi lao kwamba hawakuwa wamebeba nyama yoyote.
Tukio hilo ni jipya kabisa katika mfululizo wa
mashambulizi yanayofanywa na waumini wa Kihindu nchini humo, ambapo kumekuwa na
mlolongo wa mashambulizi dhidi ya Waislamu na watu wa jamii ya Dalit.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Waislamu
wapatao 10 wameuawa katika maeneo mbalimbali nchini humo baada ya kushukiwa
kula au kuuza nyama ya ng’ombe.
Wakosoaji wanasema kuwa magenge hayo yamechochewa na
uchaguzi wa mwaka 2014 wa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi cha Bharatiya
Janata chenye mrengo wa Kihindu.
Mwaka jana, Modi aliyakosoa magenge hayo na kutaka
udhibiti dhidi ya makundi yanayotumia dini kama kificho cha kufanya uhalifu.
0 comments:
Post a Comment