Aliyekuwa Rais wa Gambia, amewahutubia Wanagambia akieleza
kwa nini ameamua kuachia madaraka na kuitakia nchi hiyo fanaka na baraka tele.
Yahya Jammeh, ambaye aliitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka
22, ametoa maelezo hayo jana Jumamosi asubuhi - kwa majira ya nchi hiyo –
katika hotuba iliyotangazwa kwenye Redia na Televisheni ya Serikali ya Gambia (GRTS).
Katika hotuba hiyo, Bwana Jammeh alisema kuwa alifanya
juhudi kubwa kwa ajili ya nchi yake, na kuamua kuachia madaraka kwa maslahi ya
amani na usalama wa Gambia.
Alisema kuwa anaamini katika umuhimu wa mazungumzo na
alifurahi kuona kwamba mzozo wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo tangu Desemba 2016
haukusababisha kifo chochote.
Hata hivyo, kiongozi huyo hakuelezea kipi anachopanga
kufanya baadaye na iwapo ataendelea kushiriki katika siasa za taifa hilo la
Afrika Magharibi.
Hapa chini tumekuwekea hotuba kamili ya Bwana Jammeh
kama ilivyotafsiriwa na Mzizima 24.
======================
Wanagambia wenzangu,
Kazi ya kwanza kama rais, amiri jeshi mkuu wa majeshi ya
ulinzi na kama mzalendo ni kuyalinda maisha ya Wanagambia katika mazingira na
matukio yoyote. Na hili ni jukumu takatifu sana kwangu.
Daima nimefanya juhudi za kustawisha amani na usalama wa
taifa letu na bara la Afrika. Katika kipindi chote hiki ambacho Allah Subhanahu
Wa Taala kwa hekma Yake alinipa fursa na
idhini ya kuwa na madaraka, na kwa kipindi chote ambacho wananchi wa Gambia
wamekuwa na imani nami, kazi yangu ya mwanzo imekuwa ni kutetea heshima ya watu
wetu na uhuru kamili wa taifa hili adhimu.
Kutokana na juhudi mbalimbali tulizofanya sisi na wale
waliotutangulia kama taifa, Gambia imepata matlaba yake ya kustawisha
mustakbali wake na majaliwa yake. Hii ni njia ambayo muda wote nimekuwa tayari
kuitetea, hata kwa kuyatoa maisha yangu. Hatua zote tulizozichukua katika
kujenga taifa hili mpaka hapa lilipo zimetutofautisha miongoni mwa jamii ya
mataifa na kutupatia fahari ya daraja adhimu katika historia.
Pamoja na yote hayo, mimi kama Muislamu na mzalendo,
ninaamini kwamba hakuna ulazima wa tone hata moja la damu kumwagika. Tangu kuanza
kwa msuguano huu wa kisiasa ambao taifa letu adhimu linaupitia, niliahidi mbele
ya Allah Subhanahu Wa Taala na taifa
zima kuwa masuala yote yanayotukabili kwa sasa yangetatuliwa kwa amani.
Hakika ninamshukuru Allah Subhanahu Wa Taala kwamba mpaka sasa, hakuna tukio
lolote la kupoteza maisha lililotokea. Ninaamini katika umuhimu wa majadiliano
na (ninauamini) uwezo wa Waafrika wa kushughulikia sisi wenyewe changamoto zote
zinazoikabili demokrasia, maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ni kwa sababu hiyo kwamba nimeamua, kwa dhamiri njema, kulivua
joho la uongozi wa taifa hili adhimu nikitoa shukrani zangu zisizokuwa na
kikomo kwa Wanagambia wote – wanawake,
watoto, vijana na wanaume – na marafiki wa Gambia ambao wamenisaidia kuijenga
Gambia ya kisasa kwa miaka 22. Zaidi ya yote, uhuru wa watu huru wa Gambia, na
daima kwa kushirikiana nanyi nitautetea uhuru huu ambao tuliupigania kwa nguvu
zote.
Uamuzi wetu wa leo haukusukumwa na kitu kingine bali (umetokana
na) kujali maslahi yenu makuu, watu wa Gambia na taifa letu pendwa. Dua na
raghba zangu ni kuona kuwa amani na usalama vinaendelea kutawala Gambia. Katika
zama hizi ambazo tunashuhudia mizozo na vita katika maeneo mengine ya Afrika na
dunia, amani na usalama wa Gambia ni urithi wetu sote ambao tunapaswa kuulinda
na kuutetea kwa nguvu zote.
Ninaona fahari na heshima kwamba nimeitumikia nchi yetu,
Gambia. Wakati nikiwashukuru nyote, wanaume, wanawake na watoto, wanausalama
wote, raia watiifu na wale wote walioniunga mkono au waliokuwa dhidi yangu
katika kipindi chote hiki, ninawasihi wote kuweka mbele maslahi adhimu ya taifa
letu, Gambia, dhidi ya maslahi yote ya ukabila, na kufanya juhudi za pamoja
kama taifa moja kuendelea kulinda mafanikio adhimu ya nchi hii, uhuru wake,
amani, uthabiti, mshikamano na mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana katika
kipindi chote cha miaka hii.
Dua zangu ni kuiombea Gambia iendelee kuwa moja na yenye
maendeleo kwa usatwi wa kila mmoja wetu na iwe fakhari kwa watu wote.
Ninajisalimisha mbele ya hukumu ya Allah Subhanahu Wa Taaala ambaye hukumu Yake haifungwi na
ukomo wa mwanadamu, zama na historia. Allah Subhanahu Wa Taala Ndiye pekee Mwenye dhamana kuu ya
amani na haki.
Mwisho, kwa dhati na kwa moyo mmoja, ninaona fahari
kwamba nimewatumikia nyinyi na taifa letu tukufu. Ninamshukuru kila mtu kutoka
vikosi vya usalama, viongozi wa serikali, wa sasa na wa zamani, makada wa chama
changu, na zaidi kabisa ninawashukuru nyinyi watu wa Gambia, Wabunge, wa sasa
na wa zamani, kwa imani na uungaji mkono wa dhati mlionipatia.
Ninamuomba Allah Subhanahu Wa Taala aendelee kuiongoza njia yetu na
alitie nuru na baraka taifa na nchi yetu hii nzuri.
Ninachukua fursa hii kumshukuru mama yangu, mke wangu na
wanangu kwa dua na uungaji mkono walionipatia kwa kipindi chote cha miaka 22.
Ninawashukuru nyote, na ninamuomba Allah Subhanahu Wa Taala aendelee kuibariki nchi yetu.
0 comments:
Post a Comment