Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Augustine Mahiga |
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesifu
juhudi za Rais wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa juhudi za
kutanzua mgogoro wa Burundi baada ya kutua kwa muda mfupi jijini Dar es Salaam
jana usiku akitokea katika nchi za Somalia na Kenya ambapo alikwenda kwa ziara
ya kikazi, kwa mujibu wa Daily News.
“Umoja wa Mataifa unatambua kazi inayofanywa na Rais
Mkapa kuhusu suala la Burundi chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
na viongozi wake. Iwapo ukanda huu utakuja pamoja kama ilivyofanya EAC kwa
kadhia ya Burundi, nina hakika kwa pamoja wataweza kupata suluhisho la kudumu,”
alisema mkuu huyo wa UN.
Aidha, kiongozi huyo alimsifu Rais wa Tanzania kwa
utayari wake wa kuwapokea wakimbizi kutoka nchini humo, akisisitiza kazi
iliyofanywa na jumuiya za kikanda barani Afrika katika kutatua mizozo ya
kiuongozi barani humo.
Antonio Guterres alifanya mazungumzo kwa muda mfupi na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Augustine
Mahiga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mjini Dar es
Salaam.
Waziri Mahiga alimweleza mkuu huyo wa UN kuwa Mkutano
ujao wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupokea ripoti ya
maendeleo kuhusu mchakato wa amani ya Burundi. Na kama mwenyekiti wa EAC,
Tanzania ina matumaini makubwa na mchakato wa usuluhishi wa mgogoro huo chini
ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na usuluhishi wa Rais Mstaafu wa
Tanzania, Mzee Benjamin Mkapa.
0 comments:
Post a Comment