![]() |
Makamu wa Rais wa Gambia Isatou Njie Saidy |
Makamu wa Rais wa Gambia amejiuzulu kufuatia kushitadi
kwa mgogoro wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi uliochochewa na
hatua ya Rais Yahya Jammeh kukataa kung’atuka licha ya kushindwa na mpinzani
wake Adama Barrow katika uchaguzi wa mwezi Desemba.
Isatou Njie Saidy, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu
kabisa kuitupa mkono kambi ya Jammeh, alitangaza uamuzi wake huo Jumatano, saa
chache kabla ya muda wa utawala wa Jammeh kufikia tamati. Amekuwa makamu wa
rais wa Gambia tangu mwaka 1997.
Siku hiyo hiyo Waziri wa Elimu Abubacar Senghore alitangaza
kujiuzulu na kuwa waziri wa nane kuitupa mkono serikali ndani ya mwezi huu.
Awali Jammeh aliyakubali matokeo ya uchaguzi wa Desemba
1, 2016, ambapo Barrow alitangazwa kuwa mshindi, lakini baadaye akabadili
msimamo wake na kuwasilisha mashitaka yake kwenye Mahakama Kuu akilalamikia
hitilafu katika uchaguzi huo.
Nchi kadhaa za eneo hilo ambazo zimekuwa zikijaribu
kusuluhisha mgogoro huo zimetishia kuingia kijeshi iwapo Jammeh atakataa kung’atuka
pindi muhula wake wa utawala utakapofikia kikomo leo usiku wa manane.
Senegal, ambayo inaizunguka sehemu kubwa ya Gambia,
imeshapeleka vikosi kwenye mpaka wake na Gambia huku ikiziweka tayari ndege
zake za kivita ili kumg’oa Jammeh.
Wakati huo huo, Barrow ametangaza kuwa ataapishwa kama
rais halali wa Gambia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dakar, Senegal. Amekuwa
nchini Senegal tangu siku ya Jumapili baada ya viongozi wa Kiafrika wanaomuunga
mkono kumualika kuhudhuria rasmi kwenye mkutano wa mataifa hayo.
0 comments:
Post a Comment