Siku ya Jumatatu tume ya uchaguzi nchini Gambia ilionesha
kile ilichokielezea kuwa ni suluhisho la wizi wa kura na kwa wale wasiojua
kusoma wakati wa upigaji kura. Suluhisho hilo ni upigaji kura kwa kutumia
gololi.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa
nchi hiyo, Banjul, Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ilionesha ndoo tatu za bati
zinazowakilisha wagombea watatu wanaowania kiti cha urais katika uchaguzi wa
Desemba 1 katika taifa hilo dogo barani Afrika.
Wapiga kura huingia katika eneo la faragha ambalo
limezibwa ambapo hudondosha gololi moja katika mojawapo kati ya ndoo tatu
zilizopakwa rangi za na nembo za chama, na kengele hulia kuthibitisha kuwa kura
imepigwa.
![]() |
| Wafanyakazi wa tume wakisafirisha ndoo za kupigia kura zenye rangi za vyama vitatu vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Urais nchini Gambia katika mji wa Serekunda. |
“Ni kitu cha kipekee na tunajivunia,” alisema makamu
rais wa IEC, Malleh Sallah, akifafanua namna Gambia ilivyobuni wazo hilo miongo
sita iliyopita.
Maafisa wa tume ya uchaguzi wanasema kuwa mfumo huo
unafanya pasiwepo kura zinazoharibika na kuwawezesha Wagambia wasiojua kusoma
kupiga kura kwa urahisi, huku ukihakikisha kuwa kura moja pekee ndiyo
inayopigwa kwa kila mtu.
Ili kuzuia sauti ya pili kusikika, ndani ya ndoo husika
pamewekwa mchanga.
Katika matokeo ya kura yaliyotangazwa leo tume ya
uchaguzi ilimtangaza Adama Barrow, aliyekuwa akiwakilisha muungano wa vyama vya
upinzani kuwa mshindi wa kiti cha Urais huku Rais Yahya Jammeh aliyekuwa na
matumaini ya kurudi madarakani kwa mara ya tano akikubali kushindwa.
Kinyang’anyiro hicho kilikuwa na wagombea watu: Yahya
Jammeh aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 22, Adama Barrow aliyewakilisha
muungano wa vyama vya upinzani na Mama Kandeh wa chama cha Gambian Democratic
Congress (GDC) ambaye alishika nafasi ya mwisho.
Nchi hiyo ina watu 880,000 wenye sifa za kupiga kura.

0 comments:
Post a Comment