Rais Mteule wa Gambia, Adama Barrow |
Gambia haitajiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu (ICC), hayo ni kwa mujibu wa Rais mteule wa taifa hilo Adama Barrow, ambaye
amesisitiza kuwa ICC ni chachu ya utawala bora na huo ndio msingi wa utawala
wake.
Katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari la
Ujerumani (DW), Barrow amesema kuwa “hatuna haja ya kuondoka ICC”.
“Tutarudi kwenye Jumuiya ya Madola na tutakuwa sehemu ya
mashirika yote ya kimataifa,” DW imemnukuu Bwana Barrow.
“Mara tu baada ya kuingia madarakani rasmi, tutafanya
uchunguzi wa mambo mengi yaliyofanyika nchini.”
Chini ya utawala wa Rais Yahya Jamme, Gambia iliutaarifu
Umoja wa Mataifa kuwa itajiondoa ICC, na kuwa nchi ya tatu ya Kiafrika kutoa
taarifa rasmi ya kujiondoa.
Vilevile Afrika Kusini na Burundi zilipuuza wito wa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye aliziomba kurejelea uamuzi
wao na zimetuma barua kuthibitisha kuwa zinaondoka ICC.
Uamuzi wa Banjul kujiondoa kwenye mahakama hiyo ulikuwa
pigo binafsi dhidi ya mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda,
ambaye ni raia wa Gambia na Waziri wa zamani wa sheria wa nchi hiyo.
Waziri wa Habari wa Gambia, Sheriff Bojang, aliituhumu ICC
kuwa imekuwa ikiwaandama Waafrika na hasa viongozi wao huku ikifumbia macho
uhalifu unaofanywa na nchi za Magharibi.
Bwana Barrow alimshinda Jammeh katika uchaguzi
uliofanyika Desemba 1, na kuhitimisha utawala wake wa miaka 22.
0 comments:
Post a Comment