
Na Said Msonga
Utawala wa Wajerumani ulikoma Tanzania bara baada ya
Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyodumu kutoka 1914
hadi 1918.
Kuanzia mwaka 1919 hadi mwaka 1961 eneo la Tanzania bara
lilitawaliwa na Waingereza chinibya Udhamini wa Shirikisho la Mataifa na baadae
Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa.
Chini ya utaratibu huo, Tanzania bara (wakati huo
Tanganyika) haikuwa koloni kamili, bali nchi iliyowekwa chini ya mamlaka ya
kiutawala ya Uingereza (Mandated Territory).
Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye kitabu cha
Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, chini ya utawala wa Kijerumani, Tanzania bara
iliitwa Deutsche Ost-Afrika na ilikuwa lazima Waingereza kutafuta jina jingine
baada ya kushika utawala.
Leo tunaadhimisha miaka 55 tangu Tanzania Bara ipate
Uhuru wake Desemba 9, 1961.
Kulingana na taarifa iliyomo katika kitabu hicho, mwaka
1920 yalipendekwzwa majina kadhaa kwa ajili ya eneo hili linaloitwa leo
Tanzania Bara, yakiwemo majina kama "Smutsland", "Ebumea",
"New Maryland", "Windsorland" na "Victoria". Hata
hivyo majina hayo yalikataliwa na Serikali ya Uingereza kutokana na sababu
mbalimbali.
Baadae Serikali ya Uingereza ilielekeza yapendekezwe
majina ya kienyeji, ndipo yakajitokeza majina kama "Kilimanjaro" na
"Tabora" ambayo yalifikiriwa lakini hayakuchaguliwa.
Hatimaye jina "TANGANYIKA PROTECTORATE"
lilipendekezwa na msaidizi wa Waziri wa Makoloni na likakubaliwa na Serikali ya
Uingereza.
Inaelezwa kwamba , kabla ya ujio wa wazungu, wenyeji
katika maeneo ya Magharibi mwa Nchi waliliita Ziwa kubwa lililopo eneo hilo
Ziwa Tanganyika.
Inaelezwa kuwa hiyo ilikuwa ndiyo sababubkubwa
iliyofanya maofisa wa Serikali kulikubali jina la Tanganyika kwa sababu
lilikidhi matakwa ya Sera kwa kuwa lilitokana na majina ya kienyeji.
Baadae neno "Protectorate" liliondolewa kutoka
jina rasmi la "Tanganyika Protectorate" na badala yake likawekwa neno
"Territory".
Kwa hiyo kuanzia mwaka 1920 hadi Sikh ya Uhuru, eneo
ambao leo linajulikana kama Tanzania Bara, liliitwa "Tanganyika
Territory".
Pamoja na historia hiyo, Desemba 9, mwaka 1961 bendera
ya kikoloni iliyokuwa na rangi nyekundu na picha ya Twiga iliteremshwa na
bendera ya Taifa huru la Tanganyika ikapandishwa rasmi mbele ya halaiki ya
wananchi wa mji wa Dar es Salaam Mzizima.
Wakati huo huo bendera hiyo ikapandishwa juu ya kilele
cha Mlima Kilimanjaro, bendera hiyo iliyokuwa na rangi ya Kijani na Ukanda
Mweusi katikati na mistari ya Njano ilitumika kati ya mwaka 1961 hadi mwaka
1964.
Alama ya rangi Nyeusi iliwakilisha Wananchi, Njano
iliwakilisha Madini na Kijani iliwakilisha Mimea na Mazao.
Jamuhuri ya Tanganyika iliungana na Jamuhuri ya Watu wa
Zanzibar 26 Aprili, 1964 na bendera mpya ya Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar
ilianza kutumika. Katiba bendera hiyo rangi ya Bluu iliongezwa ikiwakilisha
Bahari inayounganisha Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.
Kutokana na nchi kuwa na jina refu sana la
"Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar", Serikali iliitisha shindano la
ubunifu wa jina zuri litakalotumiwa na nchi. Tangazo likatolewa kwenye gazeti
la Serikali la Tanganyika Standards (kwa sasa linaitwa Daily News).
Kijana mmoja enzi hizo aitwae Iqbal Mohamed Dar aliamua
kushiriki shindano hilo la ubunifu ambapo kwa maelezo yake anasema; Alikuwa
anapenda kwenda Maktaba Kuu ya Taifa kujisomea na ndipo alipoona tangazo la
serikali katika gazeti akaamua kushiriki, alichukua kalamu na karatasi
akaandika neno Bismillah kwa mujibu wa imani yake, kisha akaandika TAN, herufi
3 za mwanzo za jina Tanganyika, akaandika ZAN, herufi 3 za mwanzo za jina
Zanzibar kisha akaziunganisha na kupata herufi zilizosomeka TANZAN. Akazitazama
na kubaini hazina maana kamili, akaamua kuongeza 'I' herufi ya kwanza ya jina
lake Iqbal na akaongeza 'A' herufi ya kwanza ya madhheb ya dini yake ya
Ahmadiyyah na alipoziunga herufi hizo IA kwenye zile TANZAN za awali ndipo
akapata neno TANZANIA. Akamshukuru Mola wake na kuliwasilisha jina TANZANIA
Serikalini ambapo baada ya miezi kadhaa alipokea barua kutoka Wizara ya Habari
iliyosainiwa na Waziri Idris Abdul Wakil ikimtaarifu kuwa TANZANIA ndilo jina
lililoshinda na akapatiwa zawadi ya pesa Tsh 200 pamoja na Ngao. Huu ndio ukawa
mwanzo wa jina la Jamuhuri ya Muungano wa TANZANIA.
![]() |
| Mwalimu Julius K. Nyerere akiwa na wapigania uhuru wenzake |
Tukirejea nyuma kidogo tunaona Muundo na Majukumu ya
Serikali ya Tanzania Bara (Tanganyika) ilipokuwa Jamuhuri Desemba 9, mwaka 1962,
Serikali ilikuwa na Baraza la Mawaziri 11wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Mawaziri wa Serikali ya kwanza baada ya Uhuru walikuwa
ni hawa wafuatao:-
1. Rashid Mfaume Kawawa (Waziri asiye na Wizara Maalumu)
2. Oscar Kambona (Elimu)
3. Job Lusinde (Serikali za Mitaa)
4. Amir Jamal (Mawasiliano, Nguvu za Umeme na Ujenzi)
5. Nsilo Swai (Biashara na Viwanda)
6. Tewa Said Tewa (Ardhi na Upimaji)
7. Chief Abdallah Saidi Fundikira (Sheria)
8. Dereck Bryceson (Afya na Kazi)
9. Paul Bomani (Kilimo)
10. Sir Ernest Vassey (Fedha)
11. Clement George Kahama (Mambo ya Ndani ya Nchi)
Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika yalikuwepo majimbo ya
utawala 10 ambayo yalirithiwa kutoka utawala wa kikoloni wa Kiingereza.
Majimbo hayo ni Jimbo la Kati, Jimbo la Mashariki, Jimbo
la Ziwa, Jimbo la Kaskazini, Jimbo la Kusini, Jimbo la Nyanda za Juu Kusini,
Jimbo la Tanga, Jimbo la Magharibi, Jimbo la Ziwa Magharibi.
Mwaka 1966 maeneo 16 ya utawala yaliundwa yakaitwa Mikoa
ambayo ni Arusha, Pwani, Dodoma, Tanga, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya,
Morogoro, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Ziwa Magharibi.
Mwaka 1967 Mkoa mmoja wa Iringa uliundwa na kufanya
idadi ya Mikoa kufikia 17 na wilaya 60.
Serikali mpya ya Watanzania walio huru ilikuwa pia na jukumu
la kuhakikisha kuwa Huduma muhimu kwa wananchi zinapatikana na kuwahakikishia
wananchi ULINZI na usalama wa maisha yao na Mali zao. Ilitakiwa pia kujenga
mifumo ya kuendeleza Uchumi na kuanzisha mahusiano na nchi nyingine duniani na
jumuiya za kimataifa.
Miaka 55 leo bado nchi yetu inapaswa kuendelea kubaki
ikisimamia kwa vitendo misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa letu ili kuwapa
wananchi tija na unafuu wa maisha.
Nawatakia kheri na fanaka ya Miaka 55 ya Uhuru.
Makala haya yameandaliwa na ndugu Said Msonga ambaye ni
mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.

0 comments:
Post a Comment