![]() |
| Rais mteule wa Ghana Nana Akufo-Addo akizungumza na wanahabari nyumbani kwake mjini Accra, Ghana, Desemba 9, 2016. |
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Ghana cha New
Patriotic Party (NPP) ameshinda kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa
Jumatano uliokuwa na ushindani mkali huku akiahidi kuirejesha kwenye njia ya
maendeleo nchi hiyo ya Afrika Magharibi yenye utajiri wa rasilimali.
Jana jioni, Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Nana
Akufo-Addo kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 53.8 ya kura, huku Rais John
Mahama akipata asilimia 44.4. Watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia
68.6.
Akufo-Addo, ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje
na mwanasheria mkuu wa Ghana, ameshinda kiti hicho baada ya kuanguka mara tatu.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 72 ambaye ni
mwanaharakati wa haki za binadamu atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka 4
katika taifa hilo lililowahi kukoloniwa na Uingereza.
Akiwahutubia wafuasi wake nje ya nyumba yake katika mji
mkuu Accra, Akufo-Addo aliahidi kufanya kila juhudi kwa maslahi ya wananchi na
kulirejesha taifa kwenye njia ya maendeleo na ustawi.
"Sitawaangusha. Nitafanya kila lililo ndani ya
uwezo wangu kuishi ndani ya matumaini na matarajio yenu,” alisema.
Naye Rais anayeondoka madarakani, John Mahama alimpigia
simu na kumpongeza Akufo-Addo kwa kushinda kiti hicho huku akikubali kushindwa.
Ghana ambayo iliwahi kuwa na uchumi mzuri, imeshuhudia
kuporomoka kwa uchumi wake na mfumko wa bei tangu mwaka 2014 kutokana na
kuporomoka kwa bei ya mafuta, dhahabu na cocoa.
Kiwango cha ukuaji wa uchumi cha nchi hiyo kilikadiriwa
kuwa asilimia 3.3 mwaka 2016, kiwango ambacho nina chini kabisa kwa muda wa
miongo miwili.
Upinzani umemtuhumu Rais Mahama kwa kushindwa kuinua
uchumi wa nchi hiyo na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akufo-Addo ameahidi kuuamsha uchumi, kutengeneza ajira,
kujenga kiwanda katika kila wilaya ya nchi hiyo yenye wilaya zaidi ya 200 na
kutoa elimu ya sekondari ya juu bure.
Chaguzi nchini Ghana zimekuwa za amani tangu kumalizika
kwa utawala wa kijeshi mwaka 1992.

0 comments:
Post a Comment