Majeruhi wakipata huduma ya kwanza kutoka kwa maafisa wa afya mjini Bukoba mkoani Kagera. Zaidi ya watu 100 waliripotiwa kujeruhiwa. |
Watu 10 wamethibitika kupoteza maisha na wengine zaidi
ya 100 kujeruhiwa katika Wilaya ya Bukoba, Mkoani Kagera kufuatia tetemeko la
ardhi lililoikumba Kanda ya Ziwa jana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi
amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa kufuatia tukio hilo ambalo pia lilizua
taharuki kwa wananchi.
Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani, ambalo ni
shirika kubwa duniani linalofuatilia matukio kama hayo, lilisema kuwa tetemeko
hilo lilikuwa na ukubwa wa 5.7 katika Kipimo cha Richa.
Afisa Habari wa mkoa wa Mwanza, Atley Kuni alisema kuwa
watu wengi waliacha shughuli zao na kukimbilia maeneo yenye usalama.
Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani lilisema kuwa
kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa katika eneo la Nsuga, na eneo lililo jirani
na Ziwa Victoria, huku kina cha tetemeko kikiwa ni kilometa 10.
Tetemeko hilo lilitokea kilometa 29 kaskazini mashariki
mwa mji wa Kyaka, kilometa 41 kaskazini mwa Katoro, na kilometa 43 Kaskazini
Magharibi mwa mji wa Bukoba.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo pia liliripotiwa
katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara.
Aidha, Kuni alisema kuwa watu waliokuwa katika majengo
marefu, hasa katikati ya jiji la Mwanza, walilazimika kuyakimbia wakati wa
tetemeko hilo. “Taharuki na hofu iliwakumba wakazi wengi mjini na mkoa wote kwa
ujumla kwa sababu wengi wao hawakuwa wakijua kinachotokea,” alisema.
Afisa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mkoa wa
Mwanza, Augustino Nduganda alithibitisha kutoka kwa tukio hilo lakini akasema
ni mapema kutoa taarifa za kina.
“Taarifa sahihi kuhusiana na tetemeko hili zitatolewa
hivi karibuni,” alisema.
0 comments:
Post a Comment