Jenerali mmoja wa jeshi la Somalia na walinzi wapatao
wanne wameuawa baada ya msafara wao wa kijeshi kupigwa na shambulizi la bomu la
kujitoa mhanga.
Jenerali Mohamed Roble Jimale, anayejulikana pia kama "Goobaanle",
na askari kadhaa wa Kisomali wamepoteza maisha katika shambulizi hilo
lililotokea leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu, kanali wa polisi Abdikadir
Farah ameliambia shirika la habari la Reuters.
"Kulikuwa na mlipuko mkubwa uliosababishwa na gari
lililosheheni vilipuzi pembezoni mwa barabara ya viwanda, wanajeshi kadhaa
waliuawa katika tukio hilo akiwemo kamanda mwandamizi,” afisa usalama Abdiaziz
Mohamed ameliambia shirika la habari la AFP.
Mashuhuda wanasema kuwa gari hilo lilikuwa likipita
barabarani ambapo liliparamiwa na gari nyingine na kusababisha mlipuko mkubwa.
"Mlipuko ulikuwa mkubwa sana, niliona moshi ukiwa
umelifunika eneo lote,” alisema shuhuda Abdi Hassan.
Kundi la al-Shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo
katika taarifa iliyotolwa na kituo chake cha redio cha Andalus.
Taraifa hiyo inasema "mujahid [mpiganaji] amekufa
kishahidi wakati gari lake lenye bomu lilipomuua Jenerali Goobaanle".
Al-Shabab waliondoshwa katika mji wa Mogadishu na kikosi
cha walinda amani wa Umoja wa Afrika, AMISOM, mwaka 2011 lakini kundi hilo
limeendelea kuwa tishio kubwa nchini Somalia, huku likifanya mashambulizi ya
mara kwa mara yanayolenga kuiondosha serikali inayoungwa mkono na nchi za
Magharibi.
0 comments:
Post a Comment