ALAMA 7 KWAMBA MUMEO ANAIFURAHIA NDOA YENU


ALAMA 7 KWAMBA MUMEO ANAIFURAHIA NDOA YENU

Je, unataka kujua kama mumeo anaifurahia ndoa yenu? Hapa tumekuandalia orodha hii ili uangalie namna unavyoweza kuamiliana vizuri na mumeo. Kisha usiache kuwa mwenye kushukuru kwa kila jema analolifanya.

Kila mke anataka mumewe afurahie ndoa yao. Zifuatazo ni ishara na alama 7 zinazoonesha kuwa mumeo anafurahia kuwa mwanandoa:

1. BUSU
Anakupokea kwa busu anapoingia nyumbani kutoka kazini. Sio busu la haraka haraka kama mtu anayekimbizwa. Ni busu maridhawa, anakukumbatia, anakubusu kwenye kinywa chako au nyama kwa nyama. Hilo linaonesha kuwa anafurahia tena kuwa pamoja na wewe nyumbani. Hakika hiyo ni ishara ya kwamba anafurahia ndoa yenu.

2. MAWASILIANO
Mume anapotoka nyumbani kwa ajili ya shughuli zake, anawasiliana nawe kila mara na kukujulisha namna alivyo na shauku nawe. Kwa kawaida mume mwenye furaha kwenye ndoa huwa na shauku na mkewe kila anapokuwa safarini au nje ya nyumbani. Huwa na shauku mno ya kuwa pamoja nawe. Mambo atakayokwambia kwenye simu yataonesha jinsi alivyokukumbuka. Hufanya hivyo kwa dhati ya moyo wake. Daima huwa mwaminifu kwako kwa asilimia zote. Hata wewe unalijua hilo.

3. "NINAKUPENDA"
Hukwambia anakupenda. Hulisema neno hilo kila siku, na wewe humjibu. Neno hilo halichuji midomoni mwenu. Sio kama wanaume ambao wake zao hulalamika baada ya miaka mingi ya ndoa, “Huniambii kama wanipenda”, nao wakajibu, “Nilikwambia tulipooana, na kama mambo yakibadilika nitakwambia.” Hivyo sivyo mume mwenye kufurahia ndoa yake anavyofanya. Atakwambia anakupenda kwa sababu anataka ulijue hilo kila siku. Anapenda kusema hivyo kutoka moyoni mwake. Na anajua kwamba unafurahia na ni muhimu kwako kulisikia neno hilo.

4. ANAKUSAIDIA
Miongoni mwa alama za kuwa anaifurahia ndoa yenu ni kukusaidia mambo ya nyumbani. Anataka kukuangazia njia yako na kushirikiana nawe, kiasi kwamba anaweza kufanya zaidi unapokuwa hujisikii vizuri. Ni mwenza mwenye utashi katika shughuli za kuifanya nyumba yako kuwa sehemu maridhawa. Anatambua kuwa kulea watoto sio kazi yako peke yako, bali ni yake pia; yuko tayari kushirikiana nawe kwa sababu anakupenda na anawapenda pia. Kwa maneno mengine, ni mshiriki hai katika kuyafanya maisha ya nyumbani kuwa yenye furaha kwa familia yake.

5. HUKUSTAAJABIA
Mume mwenye furaha na ndoa yake hukusifu. Hukutazama na kuangalia unachofanya. Huwa makini, na utamuona mara kwa mara akikutazama na kufurahia unachokifanya. Anavutiwa na wewe, na hachoki kukutazama. Huendelea kukuona kuwa u mrembo hata kama mwili wako utabadilika kiasi gani. Haoni kasoro unazoziona. Amekuwa kipofu wa upendo na mahabba.

6. HUKUFARIJI
Hukukumbatia unapolia. Huzuni na mfadhaiko vinapokusibu na kukufanya ulie, hukufariji. Hufanya juhudi kujua tatizo linalokusibu. Daima hukupa faraja katika nyakati ngumu. Kama una busara, utaikaribisha faraja yake na kuipokea.

7. HUUFUNGUA MOYO WAKE
Hukushirikisha ndoto zake na changamoto zake. Sio rahisi kwake kufanya hivyo kama sio kwa ajili yako. Anahitaji kujua kwamba anaweza kukwambia mambo hayo bila kukusumbua, na kwamba utamuunga mkono na kumfanya ajiamini. Anapokuwa tayari kuunfungua moyo wake na kukwambia mipango na matarajio yake kuhusu shughulizake, anatambua kuwa utasikiliza na kujali. Anatambua kuwa wewe ni shabiki wake namba moja. Anajua pia kwamba upendo wake kwako ni wa dhati na utakufanya uelewe na kutaka kujua kuhusu wasiwasi wake. Mume mwenye furaha katika ndoa yake anaweza kufanya hivyo kwa kujiamini kabisa.

WITO

Wito wangu kwa wanaume wanaosoma somo hili tamu: Iwapo hamfanyi haya, sasa ni wakati wa kuanza kuwafanya wake zenu kuwa vipaumbele vyenu. Hamjachelewa kutengeneza furaha katika ndoa zenu.

Wito wangu kwa wanawake wanaosoma somo hili, furahieni mazuri yote yanayofanywa na waume zenu. Pia wafanyeni kuwa vipaumbele vyenu, mtakuwa miongoni mwa wanandoa wenye furaha watakaoithibitishia dunia kwamba ndoa na furaha ni mapacha wasiotenganishwa, hata katika nyakati ngumu.

Ungana nasi kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment