Aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula na Kada mkongwe wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira ameomba wasaidizi wa Rais John
Magufuli kumshauri kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kuepusha
madhara yanayoweza kutokea kutokana na
maandamano yanayopangwa kufanyika Septemba 1.
Wassira ameeleza kuwa washauri hao wanapaswa kufanya
hivyo kwani bado nafasi hiyo ipo kuliko kuacha Rais aingie vitani na wananchi
wake kwani madhara yatawapata Watanzania wote.
“Wazungumze ili wasimuingize Rais kupigana na watu wake
kwa maana wote tutapoteza. Kwa nini uweke askari polisi wote hao, msimweke Rais
kwenye vita na watu wake,” Wassira anakaririwa na Jambo Leo.
“Kinachohitajika ni wasaidizi wa Rais kumshauri ili
kuhakikisha kuwa tofuati zilizopo baina yake na vyama vya upinzani haziendelei
ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika, itafutwe suluhu,”aliongeza.
Akizungumzia uamuzi wa Serikali kupiga marufuku
kufanyika kwa mikutano na maandamano, alisema kuwa tatizo linaweza kuwa ni
aliyekuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Alisema kuwa hii inatokana na joto la uchaguzi
lililokuwepo pamoja na nia ya Lowassa kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga
kura, kungeweza kuzua tafrani kubwa kwani alipata kura nyingi na alikuwa akidai
ameshinda kwa asilimia 62.
“Ukiwaruhusu kufanya mikutano na ukwaambia kuwa
atakayekuja kutoa shukurani ni Lowassa, ambaye amekuwa akipinga kushindwa ni
sawa na kurejesha hali ya uchaguzi kipindi hiki,” alisema.
Alitaka Serikali kutoa elimu ya wazi kwa umma kuhusu
sababu zinazopelekea kukataza kufanyika kwa mikutano ili kuweka mambo sawa.
“Kama mimi hapa nimetaja sababu kwamba inawezakana kuwa
ni Lowassa. Sasa na wao Serikali waseme tu tunapiga marufuku mikutano na
maandamano… wataje [sababu] na kuzifafanua,” alieleza.
Hata hivyo, Wassira aliwataka Chadema kusitisha azma yao
na kuhakikisha wanafuata utaratibu ili kupata haki ya kufanya maandamano na
mikutano ambayo alieleza kuwa kila Katiba ya nchi duniani imeiweka, lakini bila
kufuata utaratibu haiwezi kuruhusiwa.
Ungana nasi katika group ya WhatsApp kupitia: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment