CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Dar
es Salaam, kimemkaribisha Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro
kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kwenye maandamano ya Operesheni Ukuta
yatakayofanyika Septemba Mosi.
Kimesema kinamkaribisha kamanda huyo ili kuondoa uwezekano
wa kupelekewa taarifa za uongo na askari wake kuhusu maandamano hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam,
Benard Mwakyembe, alisema jana kuwa hakuna haja ya kamanda huyo kukaa ofisini
bali ajitokeze katika Operesheni Ukuta na awe mstari wa mbele kuwapiga wananchi
ambao watatumia muda huo kumuuliza maswala ya sheria kuhusu maandamano hayo.
“Lengo la Operesheni Ukuta ni kuwaeleza wananchi kuwa
nchi yetu haifuati sheria bali inafuata mawazo ya mtu mmoja.
“Tumwambie tu kwamba Kamanda Sirro ngoma hii ya Ukuta si
ya kitoto, vitisho na mbwembwe zake anazozionyesha barabarani hazitutishi, tupo
tayari kwa lolote.
“Tumejiandaa kisaikolojia kwa namna yoyote, tupo tayari
kufa kwa ajili ya kuwatetea wananchi, na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya
Mwita, atakuwa mstari wa mbele pamoja na viongozi wengine,” alisema Mwakyembe.
Aidha alisema maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia
99.5 katika mitaa 582 na kata 102 ya jiji zima la Dar es Salaam.
“Niwashukuru Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UV-CCM) kwa kutuunga mkono kuandaa maandamano yao, tunaamini haya ya kwetu
yamewapa motisha na kuamua kufanya ya kwao.
“Ninaliomba Jeshi la Polisi liwape ulinzi wa kutosha
ingawaje sisi tunajua kwamba huo ni mtego walioufanya kisiasa ili kuleta mabishano
ambayo hayana nafasi kwetu,” alisema.
Alisema haki za vyama vya siasa ni kutoa maoni ya
kisiasa kadiri vitakavyoona inafaa, ili
kutekeleza sera zake kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment